Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YAENDELEZA ELIMU YA VIWANGO NANENANE, YAWAFUNGULIA WAZALISHAJI MASOKO


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini limeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane 2026 kutoa elimu kwa wazalishaji, wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango ili kuongeza tija na kupanua masoko ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza katika Maonesho hayo Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, amesema TBS inashiriki katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Uwanja wa Makangale, Mbeya, kwa lengo la kutekeleza jukumu lake la kutoa elimu na huduma za viwango kwa wadau mbalimbali wanaoshiriki maonesho hayo.

Amesema ushiriki wa TBS unaendana na kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane ya “Tambua Soko, Ongeza Tija ili Kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050,” kwa kuwa viwango ni sehemu muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi mahitaji ya masoko mbalimbali.

“Tunazungumzia wazalishaji mbalimbali, wauzaji na wale wanaosafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi. Wote wanahitaji kukidhi viwango. Tunapotoa elimu hii tunawaongezea fursa ya kupata masoko mapana zaidi, siyo Tanzania pekee bali pia katika Afrika Mashariki na soko la Afrika,” amesema Alananga.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, TBS inaendelea kuimarisha utekelezaji wa dira yake ya kuwa taasisi inayoongoza barani Afrika katika masuala ya viwango bora na usalama, huku ikiendelea kuhakikisha wazalishaji wanapata uelewa unaowawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na ushindani.

Amesema pamoja na kutoa elimu, TBS inatoa huduma mbalimbali moja kwa moja katika maonesho hayo, ikiwemo usajili wa maeneo ya biashara za vyakula.

Ameeleza kuwa huduma hiyo ni muhimu katika kuhakikisha maeneo yanayohusika na uuzaji wa vyakula, yakiwemo maduka ya rejareja, supermarket na migahawa, yanakidhi masharti yanayolenga kulinda afya za walaji.

“Tunatoa huduma za usajili wa maeneo ya chakula. Wale wote wanaofanya biashara za kuuza bidhaa za chakula kwenye maduka ya rejareja, supermarket na migahawa tunaweza kuwahudumia hapa na kupata usajili wao,” amesema.

Aidha, Alananga amesema TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeanza rasmi kutoa huduma ya metrologia, inayohusisha upimaji na uhakiki wa vifaa na vipimo mbalimbali vinavyotumika katika maeneo kama maabara, viwandani, hospitalini na kwenye sekta ya ujenzi.

Amesema huduma hiyo ni miongoni mwa huduma mpya zinazotolewa na ofisi hiyo baada ya maabara na huduma husika kupata ithibati kutoka Makao Makuu ya TBS jijini Dar es Salaam.

“Huduma hii mwaka huu rasmi tumeanza kuitoa hapa katika ofisi ya Nyanda za Juu Kusini. Tunaamini wako wadau mbalimbali ambao walitarajia kupata huduma hii, lakini walikuwa wakiipata kupitia Makao Makuu. Sasa tumeisogeza Mbeya ili iwe rahisi kuwahudumia,” amesema.

Ameeleza kuwa huduma hiyo inawahudumia wadau kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Njombe, huku TBS ikiwa na uwezo wa kuwafikia pia wadau kutoka mikoa jirani ikiwemo Katavi na Ruvuma.

Kwa upande mwingine, amesema TBS inatoa huduma za uthibitishaji wa bidhaa na kuwawezesha wajasiriamali pamoja na viwanda kupata alama ya ubora ya TBS, hatua ambayo inaweza kuongeza uaminifu wa bidhaa na kusaidia wazalishaji kuingia katika masoko mapana.

Alananga amewataka wazalishaji na wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Nanenane kutumia fursa hiyo kutembelea banda la TBS ili kupata elimu kuhusu viwango, taratibu za uthibitishaji na huduma nyingine zinazotolewa na shirika hilo.

Amesema TBS pia imeweka utaratibu maalumu wa kuwafikia wajasiriamali wadogo katika mabanda mbalimbali ya maonesho hayo, badala ya kusubiri wao kufika katika banda la shirika hilo.

“Tumeweka huduma maalumu kwa ajili ya wajasiriamali wadogo. Tunawatembelea kwenye kila banda mmoja mmoja ili kuwapa elimu na kuwasaidia kuelewa namna ya kuthibitisha bidhaa zao,” amesema.

Amewapongeza wazalishaji ambao tayari bidhaa zao zimepata uthibitisho wa TBS na kuwataka wale ambao bado hawajathibitisha bidhaa zao kutumia fursa hiyo kupata elimu na kuanza mchakato wa uthibitishaji.

Amesema lengo ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zinakuwa na uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

“Tunatamani bidhaa zote zinazoshiriki katika maonesho haya, hasa zile ambazo bado hazijathibitishwa, zipate elimu. Tunaamini elimu hii itawasaidia kupenya katika masoko ya maonesho mengine makubwa zaidi, ndani ya nchi na hata nje ya nchi,” amesema Alananga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com