Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AIELEKEZA TAMISEMI KUSIMAMIA HUDUMA ZA UGANI KWA TIJA NA UFANISI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuhakikisha Wakala wa Huduma za Ugani (NAESA) unatekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi, huku ukizingatia dhana ya ugatuaji wa madaraka, maarufu kama D by D.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo Agosti 08, 2026 wakati kufunga rasmi Maonesho ya Nane Nane Kitaifa na Kimataifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma.

Aidha, Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuendelea kushughulikia na kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Amesisitiza kuwa makundi hayo yote mawili yana umuhimu mkubwa katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo ni muhimu kuweka mazingira yatakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa amani na tija.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu OWM-TAMISEMI, anayeshughulikia masuala ya Afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao, hususan kupitia fursa zinazotolewa na Serikali za Mitaa.

“Tumefanya vizuri kupitia mikopo ya halmashauri kuwafikia wananchi wengi na kuongeza uzalishaji, lakini bado kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi kwa kuwafikia vijana wengi, kina mama wengi na watu wenye ulemavu ili waingie katika mnyororo mzima wa uzalishaji,” amesema Prof. Nagu.

Aidha, Prof. Nagu amesema kuongeza tija katika kilimo hakupaswi kuishia katika uzalishaji wa mazao pekee, bali kunapaswa kuhusisha hatua zote za mnyororo wa thamani, ikiwemo uzalishaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji na upatikanaji wa masoko.

Amesema Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, kutoa elimu, kuonesha teknolojia na ubunifu katika uzalishaji, pamoja na kujadili fursa zinazoweza kuongeza tija na thamani katika sekta ya kilimo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com