Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Jitihada za Serikali za kuongeza tija, uzalishaji na uwekezaji katika sekta ya kilimo zimeendelea kupata msukumo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji na wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
Kutokana na mchango huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, ameipongeza TADB wakati alipotembelea banda la benki hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, akisema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ya kilimo kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi.
Amesema huduma zinazotolewa na TADB zimeendelea kuwafikia wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha thamani ya mazao na mifugo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wananchi.
Katika ziara yake leo Agosti 6,2026 ,Mhe. Chande amepata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo mikopo kwa wakulima, wafugaji na wawekezaji wa sekta ya kilimo, pamoja na programu maalumu zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zinazowekeza katika maendeleo ya kilimo kwa kuwa sekta hiyo ndiyo mhimili wa uchumi wa taifa na chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa mamilioni ya Watanzania.
Kwa upande wa TADB imeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kuhusu huduma zake za kifedha, kuhamasisha uwekezaji katika kilimo na kuwafikisha karibu zaidi wadau wanaohitaji mitaji ya kukuza shughuli za uzalishaji na biashara za kilimo.


Social Plugin