Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BIMA YA AMANA YATOA UHAKIKA WA USALAMA WA FEDHA ZA WAWEKAJI BENKI



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Wananchi wametakiwa kuendelea kutumia huduma za benki kwa kujiamini baada ya Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kueleza kuwa mfumo wa bima ya amana unalinda fedha za waweka amana endapo benki au taasisi ya fedha itashindwa kuendelea na shughuli zake na kufutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akizungumza Agosti 6,2026 katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana, Lwaga Mwambande, amesema kila mteja anayefungua akaunti katika benki yenye leseni ya BoT hunufaika na kinga hiyo bila kulazimika kuchangia moja kwa moja.

Amesema kwa sasa kiwango cha juu cha fidia kinacholipwa na Bodi hiyo ni shilingi milioni 7.5 kwa kila mwekaji amana, hivyo iwapo benki itafutiwa leseni na kushindwa kuendelea na shughuli zake, wateja wenye amana zisizozidi kiwango hicho hulipwa fidia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Mwambande amefafanua kuwa Mfuko wa Bima ya Amana huchangiwa na benki na taasisi za fedha wanachama wa mfumo huo, ambazo hutoa mchango wa asilimia 0.15 ya amana zao zote kwa mwaka.

Amesema fedha zinazokusanywa huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine salama ya uwekezaji ili kuimarisha uwezo wa mfuko kulipa fidia pale inapohitajika.

Aidha, amesema wateja wenye amana zinazozidi kiwango cha fidia hawapotezi fedha zao zote, kwani baada ya benki kufungwa huanza mchakato wa ufilisi ambapo mfilisi aliyeteuliwa kwa mujibu wa sheria hukusanya mali za benki na kuzigawa kwa wadai kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

Mwambande amesema pamoja na kulipa fidia, Bodi ya Bima ya Amana pia ina jukumu la kusaidia kupunguza hasara kwa benki zinazokumbwa na changamoto za kifedha kabla hazijafikia hatua ya kufungwa.

Amesema hatua hizo zinaweza kujumuisha kutoa mtaji, dhamana au mikopo kwa benki husika ili kuziwezesha kurejea katika hali ya kawaida, jambo ambalo mara nyingi huwa na gharama ndogo kuliko kusubiri benki ifungwe na kuanza kulipa fidia kwa wateja.

Kwa mujibu wake, majukumu makuu ya Bodi hiyo ni kukusanya michango kutoka kwa benki wanachama, kuwekeza fedha za mfuko wa bima ya amana, kulipa fidia kwa wateja wa benki zilizofungwa, kusimamia ufilisi pamoja na kupunguza hasara kwa benki na taasisi za fedha zenye changamoto.

Kwa upande wake, Meneja wa Fedha na Uhasibu wa Bodi ya Bima ya Amana, Romuli Mtui, amesema jumla ya benki tisa zimewahi kuwekwa chini ya ufilisi nchini, huku mchakato wa baadhi yake ukiendelea.

Amezitaja benki hizo kuwa ni Greenland Bank iliyofungwa mwaka 2000, Delphi Bank mwaka 2003, pamoja na FBM Bank, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank, Kagera Farmers' Cooperative Bank, Efatha Community Bank na FDM Bank zilizofutiwa leseni mwaka 2017 na 2018.

Mtui amesema michakato ya ufilisi huchukua muda kutokana na uwepo wa mali, wadaiwa, wadai na wakati mwingine mashauri yanayofikishwa mahakamani kabla ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria.

Ameongeza kuwa Bodi imeendelea kulipa fidia kwa wateja wa benki zilizofungwa, na hivi karibuni ilitangaza malipo ya mwisho ya fidia kwa baadhi ya wateja wa FDM Bank.

Amewataka wateja ambao bado hawajachukua fedha zao kufuatilia malipo hayo kupitia ofisi za Bodi ya Bima ya Amana zilizopo ndani ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam na Dodoma au kutumia njia rasmi za mawasiliano za Bodi hiyo.

Pia amewahimiza wateja wenye amana zilizozidi kiwango cha fidia kuendelea kufuatilia taratibu za ufilisi ili waweze kulipwa fedha zinazostahili kutokana na mali zitakazopatikana katika mchakato huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com