Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alipotembelea banda la wakulima katika Maonesho ya 8 8 Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika katika Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya 
Na Regina Ndumbaro-Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ameitaka TANROADS na TARURA Mkoa wa Mbeya kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi ya barabara ili kuifanya Mbeya kuwa Jiji lenye miundombinu inayoendana na hadhi yake kama makao makuu ya Nyanda za Juu Kusini.
Mrindoko ametoa agizo hilo wakati alipotembelea banda la wakulima katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya, ambako alipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya barabara kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga.
Amesema barabara nzuri ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kuwa hurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda masoko, huku pia zikisaidia kupunguza vumbi, kurahisisha upitishaji wa vyombo vya moto na kuboresha muonekano wa Jiji la Mbeya.
Amesisitiza kuwa Jiji hilo, kutokana na hadhi yake na nafasi yake katika Nyanda za Juu Kusini, linapaswa kuwa na miundombinu bora inayokidhi mahitaji ya wananchi.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imekubaliana na wabunge wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine na kupelekwa Hazina zinaelekezwa moja kwa moja kwenye mfuko wa barabara.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara za njia nne na kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi katika usafiri.
Balozi Omar amebainisha kuwa kupitia takriban mifuko saba ya ujenzi, Serikali imepanga asilimia 70 ya fedha za mifuko hiyo kuelekezwa moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. Hatua hiyo, amesema, inalenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, kuboresha usafiri na usafirishaji wa mazao na mizigo, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Mbeya na maeneo jirani.
Kwa upande wa wananchi wa Mkoa wa Mbeya akiwemo Elia Mwashilindi mkazi wa Mbalizi na Rahabu Njenzya wamesema wanaishukuru Serikali kwa kuwaletea fedha hizo ili waondokane na kadhia wanazozipata hasa baadhi ya maeneo kuwa si rafiki wakati wa msimu huu wa kiangazi baadhi ya barabara kuwa na vumbi na hata kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara zao jirani na barabara hizo kupata changamoto
"Tunaishukuru Serikali tunaamini mradi huu ukikamilika sisi wananchi na wafanyabiashara tutaweza kusafirisha bidhaa zetu kwa urahisi nahata kwa hawa wenzetu wa wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara wataondokana na changamoto hii ya vumbi"


Social Plugin