Na Mbuke Shilagi - Kagera.
Wafanyabiashara wapya mkoani Kagera wamepokea kwa matumaini mabadiliko yanayohusu msamaha wa kodi kwa kipindi cha miezi 12, wakisema hatua hiyo inaweza kuwa fursa muhimu ya kuimarisha biashara zao kabla ya kuanza kutimiza wajibu wa kulipa kodi.
Hayo yameelezwa leo Agasti 18,2026 wakati wa semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera kwa wafanyabiashara katika Ukumbi wa St. Teresa, Manispaa ya Bukoba, ikiwa na lengo la kuwafahamisha mabadiliko ya sheria za kodi yaliyomo katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027.
Mfanyabiashara Grace Pantaleo amesema msamaha huo wa miezi 12 ni fursa inayoweza kuwasaidia wafanyabiashara wanaoanza biashara kupata muda wa kujipanga na kuimarisha misingi ya biashara zao.
Amesema badala ya kuona kipindi hicho kama nafasi ya kukwepa wajibu wa kodi, wafanyabiashara wanapaswa kukitumia kama muda wa kufanya maandalizi na kujenga uwezo wa biashara ili baada ya miezi 12 wawe tayari kuanza kulipa kodi kwa ufanisi.
Mtazamo huo umeungwa mkono na mfanyabiashara Jojina Jonathan Kagisa, ambaye amepongeza TRA kwa kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwapatia elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi.
Grace amesema semina hiyo imewasaidia wafanyabiashara kufahamu mabadiliko mapya na changamoto zinazoweza kujitokeza, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa programu za elimu ili wafanyabiashara wasibaki nyuma katika uelewa wa sheria.
Kwa upande wake, Meneja wa Chemba ya Taifa ya Biashara Mkoa wa Kagera, Bw. Rweyechungura Mali, ameipongeza TRA kwa kutoa elimu hiyo, akisema uelewa wa sheria ni muhimu katika kujenga mazingira ambayo wafanyabiashara wanaweza kutekeleza wajibu wao bila kuona kodi kama kikwazo.
Bw. Mali ametoa wito kwa TRA kuchukua kwa uzito mapendekezo yatakayotolewa na wafanyabiashara na kuyafanyia kazi pale inapobidi, ili changamoto zitakazobainishwa ziweze kupata ufumbuzi.

















Social Plugin