Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewahimiza wateja waliokuwa na amana katika benki na taasisi za fedha zilizofungwa kujitokeza haraka kuwasilisha madai yao ya fidia, ikibainisha kuwa mamia ya wanufaika bado hawajafika kudai fedha zao licha ya utaratibu wa malipo kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Isack Nikodem, alisema bado kuna wateja 428 ambao hawajawasilisha madai yao, hivyo akawataka kutumia fursa hiyo ili waweze kulipwa stahiki zao kwa wakati.
Alifafanua kuwa wateja waliokwisha wasilisha madai na kulipwa asilimia 85 ya fidia hawana sababu ya kuwasilisha maombi mapya, kwani taarifa zao tayari zipo kwenye mfumo wa DIB na malipo yaliyosalia yataingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zao mara taratibu zitakapokamilika.
Nikodem alisema DIB imeendelea kuboresha mifumo yake ili kuhakikisha walengwa wanapata fidia kwa haraka pindi benki au taasisi ya fedha inaposhindwa kuendelea na shughuli zake kutokana na kufilisika au kufungwa kwa mujibu wa sheria.
Alieleza kuwa DIB ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kulinda amana za wateja katika benki na taasisi za fedha zilizo chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuhakikisha wawekaji amana hawapotezi fedha zao pale taasisi hizo zinaposhindwa kuendelea na shughuli zake.
Kwa mujibu wa sheria, alisema kiwango cha juu cha kinga ya amana kwa sasa ni Sh milioni 7.5 kwa kila mteja mwenye sifa za kulipwa fidia.
Aidha, alibainisha kuwa fedha zinazotumika kulipa fidia hazitokani na bajeti ya Serikali, bali hutokana na michango maalumu inayotolewa na benki pamoja na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania, kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kisheria.
Alisema mfumo huo wa uchangiaji umeiwezesha DIB kutekeleza wajibu wake wa kulinda imani ya wananchi katika sekta ya fedha na kuhakikisha wawekaji amana wanaendelea kuwa na uhakika wa usalama wa fedha zao hata pale taasisi wanazozitumia zinapokumbwa na changamoto.




Social Plugin