Takribani wakulima wadogo 1,000 kutoka mikoa ya Morogoro, Dodoma na Arusha wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya kuondokana na matumizi ya viuatilifu hatarishi katika shughuli zao za kulimo.
Idadi hiyo ya wakulima itawagusa moja kwa moja wakulima wa mbogamboga, vitunguu, mbogamboga na pamba waliopo kwenye wilaya za Karatu, Chamwino, Mvomero na Meru.
Hatua hiyo inayolenga kuwahamasisha wakulima kuachana na matumizi ya viuatilifu hatarishi ili kupunguza madhara ya kiafya yanayosababishwa na kemikali hizo kuanzia kwa mkulima mpaka kwa mlaji.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Asasi Isiyo ya Kiserikali ya AGENDA For Environment and Responsible Development, Dorah Swai, mkoani Morogoro wakati wa warsha ya siku mbili ya wadau wa kilimo bora na mazingira kutoka katika taasisi za serikali na binafsi.
Bi. Swai amesema kuwa mradi huo uliofadhiliwa na mfuko wa Global Frame Work (GFC) unahusisha nchi tatu za ukanda wa Mahariki mwa Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya na Ethiopia na kila nchi imejiwekea malengo ya kufikia angalau wakulima 1000.
Amesema dhamira kuu ya mradi huo wa kuondoa viuatilifu hatarishi ukanda wa Mashariki mwa Afrika una lengo la kuangalia namna bora ya kuwawezesha wakulima wadogo 3,000 watakaokuwa vinara wa mabadiliko katika matumizi ya viuatilifu mbadala kwa wenzao.
Katika warsha hiyo, Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Kiwango, amesema serikali iko tayari kushiriukiana na wadau wote wenye nia ya kuwainua Watanzania kupitia sekta ya kilimo kinachozingatia utunzaji wa mazingira na afya za binadamu.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Asasi ya Mwavuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bakari Mongo, pamoja na Afisa Programu Mkuu wa Agenda, Silvani Mng’anya, kila mmoja kwa nyakati tofauti amesema suala la kupambana na viuatilifu hatarishi halipaswa kuwa la mtu mmoja au kikundi Fulani, kwani madhara ya viuatilifu hatarishi hayaishii kwa mtu mmoja.
“Jukumu la kuondoa viuatilifu hatarishi halipaswa kuwa la mtu mmoja, ni jukumu letu sote katika kuhakikisha mlaji wa mwisho analindwa dhidi ya madhara yatokanayo na viuatilifu hatarishi.”amesema Mongo.



Social Plugin