Waandishi wa Habari wa redio ya vijana Bongo FM wameishukuru Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa kuwajengea uwezo na kuwakumbusha masuala mbalimbali ya taaluma kupitia mafunzo ya siku tatu yaliyolenga kuimarisha weledi katika utendaji wao.
Mafunzo hayo yalifanyika Julai 29-31, 2026, katika Ofisi za JAB jijini Dar es Salaam na kuhusisha mada mbalimbali zikiwemo Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari, uzalendo pamoja na mbinu bora za uandishi na utangazaji wa habari.
Akitoa salamu za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakati wa tathmini ya mafunzo hayo, Meneja Huduma za Biashara Redio-TBC, Bi. Stella Setumbi, amesema Shirika linaamini mafunzo hayo yatatoa mchango chanya katika utekelezaji wa shughuli za kihabari za watumishi hao, ikiwemo kuondoa makosa ya kimaadili katika uandishi wa habari.
Bi. Stella amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kuendelea kusisitiza uzingatiaji wa weledi katika taaluma ya uandishi wa habari huku akiwahimiza watumishi kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kutoa taarifa zinazojenga jamii yenye maadili.
Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo, Mkuu wa Bongo FM, Bi. Annastazia Willherick ameishukuru JAB kwa kuichagua redio hiyo kuwa miongoni mwa vyombo vya kwanza kupata mafunzo hayo.
“Tunaishukuru sana Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kwa kuchagua kuanza na sisi Bongo FM. Ili uwe bora, lazima upate mafunzo ya mara kwa mara. Mafunzo haya yametuongezea uelewa mkubwa kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari na uzalendo.
Pia, tumeelewa namna ya kuandika na kutangaza habari kwa kuzingatia sheria ili kuepuka kuingilia haki na uhuru wa watu wengine,” amesema Bi. Annastazia.
Ameongeza kuwa Waandishi wa Habari, hususan vijana, wanapaswa kuandika habari zinazolinda maslahi ya Taifa na kuchangia maendeleo badala ya kuharibu taswira ya nchi.
Naye, Mwandishi wa Habari wa Bongo FM, Anord Philmon, amesema mafunzo hayo yamemkumbusha wajibu wake kama Mwandishi wa Habari na umuhimu wa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, maadili na maslahi ya umma.
Kwa upande wake, Mwandishi wa Habari wa Bongo FM, Irene Kilango, ameahidi kuyafanyia kazi maarifa aliyoyapata, akieleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kutambua makosa yanayofanywa na baadhi ya Waandishi wa Habari, ikiwemo kutowatendea haki vyanzo vya habari na kuchafua watu bila kufuata misingi ya taaluma.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB Wakili Patrick Kipangula ameeleza kuwa Bodi itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa Waandishi wa Habari nchini mara kwa mara. Katika kuhitimisha mafunzo ya siku tatu, washiriki wote wametunukiwa vyeti vya ushiriki.


Social Plugin