Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Tanzania inaunga mkono mapendekezo ya marekebisho ya Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki yanayolenga kukomesha biashara ya zebaki duniani na kuweka mwaka 2032 kuwa mwisho wa matumizi ya kemikali hiyo katika uchimbaji mdogo wa dhahabu (ASGM), hatua inayotarajiwa kulinda afya za wananchi, mazingira na vizazi vijavyo.
Msimamo huo umeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kupunguza athari za zebaki, kemikali inayotajwa kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na mazingira, huku sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu ikiendelea kuwa mtumiaji mkuu wa kemikali hiyo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa Julai 30, 2026, jijini Dodoma katika warsha ya wadau wa mazingira iliyojadili mapendekezo ya marekebisho ya Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki, yakilenga kukomesha biashara ya zebaki duniani na kuweka mwaka 2032 kuwa mwisho wa matumizi yake katika sekta ya ASGM.
Akizungumza katika warsha hiyo, Afisa Programu wa AGENDA, Angel Shaniva, alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia Mkataba wa Minamata, bado dunia inakabiliwa na changamoto mbili kubwa ambazo ni kuendelea kwa biashara ya zebaki na kutokuwepo kwa tarehe rasmi ya kusitisha matumizi yake katika uchimbaji mdogo wa dhahabu.
Amesema kwa mujibu wa muhtasari wa sera wa mradi wa marekebisho ya Mkataba wa Zebaki ulioandaliwa na IPEN, marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuzuia biashara ya kimataifa ya zebaki isipokuwa kwa matumizi yanayokubalika kimazingira kama vile uhifadhi na utupaji salama.
"Marekebisho hayo yatasaidia kufunga njia zinazowezesha zebaki kuingia katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu. Pendekezo jingine ni kuweka mwaka 2032 kuwa mwisho wa matumizi ya zebaki katika sekta ya ASGM ili nchi ziwe na ratiba maalumu ya kuachana na kemikali hiyo," amesema Shaniva.
Ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 153 wanachama wa Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki, unaolenga kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara ya kemikali hiyo.
Aidha amesema matumizi ya zebaki nchini yanaendelea kuhusishwa zaidi na uchimbaji mdogo wa dhahabu katika maeneo mbalimbali ikiwemo Geita, Shinyanga, Mbeya na Mara, ambako wachimbaji hutumia kemikali hiyo kutenganisha dhahabu na mchanga.
Kwa mujibu wake, matumizi hayo husababisha uchafuzi wa ardhi na vyanzo vya maji, kuathiri samaki na usalama wa chakula, pamoja na kusababisha madhara ya kiafya ikiwemo uharibifu wa mfumo wa fahamu.
Shaniva amesema takwimu za biashara ya zebaki duniani imeongezeka kutoka tani 1,200 mwaka 2017 hadi tani 1,700 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 40, huku sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu duniani ikitumia zaidi ya tani 2,000 za zebaki kila mwaka.
Amesema nchini Tanzania zaidi ya watu milioni 1.2 wanajihusisha moja kwa moja na uchimbaji mdogo wa dhahabu, wakati takribani watu milioni 7.2 wanategemea sekta hiyo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
"ASGM inachangia takribani asilimia 40 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini na kutoa karibu asilimia 90 ya ajira katika sekta ya madini. Wanawake ni kati ya asilimia 20 hadi 30 ya nguvu kazi katika sekta hiyo," amesema
Kwa upande wake, Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Tawfiq Halfan, alisema kuondoa matumizi ya zebaki kutalinda wachimbaji, wanawake na watoto dhidi ya madhara ya sumu ya kemikali hiyo, pamoja na kuhifadhi mazingira na kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini.
Amesema kuunga mkono marekebisho hayo katika mkutano wa COP7 kutadhihirisha dhamira ya Tanzania ya kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Minamata na kuongeza kasi ya hatua za kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.
Mradi wa marekebisho ya Mkataba wa Zebaki unaotekelezwa na AGENDA kwa kushirikiana na wanachama wengine wa IPEN unalenga kuongeza uelewa kwa serikali, wabunge, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari kuhusu hatua zinazohitajika ili kupunguza na hatimaye kukomesha matumizi ya zebaki nchini.
Kwa kuunga mkono mapendekezo hayo, Tanzania inajiweka katika nafasi ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu kwa kutumia teknolojia mbadala salama, huku ikichangia juhudi za kimataifa za kuondoa matumizi ya zebaki na kulinda afya ya binadamu pamoja na mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.



Social Plugin