Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTOKUWA KIKWAZO KWA WAWEKEZAJI



Na Mwandishi wa OTR Pwani.

Serikali imezitaka Taasisi za Umma kuhakikisha zinakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji kupitia mifumo yenye ufanisi, kupunguza urasimu usio wa lazima, kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika kuunga mkono utekelezaji wa Dira 2050.

Wito huo ulitolewa Ijumaa jioni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, wakati akifunga awamu ya tatu ya Programu ya Mafunzo Elekezi ya siku nne kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na viongozi hao, Mhe. Kikwete alisema mafanikio ya Dira 2050 hayatategemea ubora wa sera na mipango pekee, bali namna taasisi za umma zitakavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuzalisha matokeo yanayoonekana kwa wananchi na kwa uchumi wa Taifa.

Amewataka Wakuu wa Taasisi za Umma kuhakikisha taasisi wanazoziongoza zinachangia kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji kupitia utoaji wa huduma wenye ufanisi, ubunifu na ushirikiano mkubwa na sekta binafsi.

Alisema taasisi za umma zinapaswa kuwa wawezeshaji wa maendeleo badala ya kuwa vikwazo kwa wawekezaji, kwa kuwa ubora wa huduma zinazotolewa una mchango mkubwa katika kuvutia uwekezaji, kuongeza ushindani wa uchumi na kufungua fursa mpya za maendeleo.

Alisisitiza kuwa uongozi wa Watendaji Wakuu utapimwa kwa uwezo wao wa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara na uwekezaji, kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza tija na kujenga taasisi zinazowajibika kwa wananchi.

"Uongozi wenu utapimwa si kwa mipango mizuri pekee, bali kwa uwezo wa kuitekeleza, kuondoa urasimu usio wa lazima, kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza tija na kujenga taasisi zinazowajibika kwa wananchi," alisema.

Aliongeza kuwa kila taasisi ya umma inapaswa kutambua kuwa maamuzi yake yana athari ya moja kwa moja katika mazingira ya biashara na uwekezaji, hivyo kila mchakato wa utoaji huduma unapaswa kujenga imani kwa wawekezaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

"Wajibu wenu wa msingi ni kuhakikisha Dira 2050, iliyoanza kutekelezwa rasmi Julai Mosi mwaka huu, inageuzwa kuwa matokeo yanayoonekana kupitia taasisi mnazoziongoza,” alisema.

“Nina matarajio kuwa utekelezaji wa Dira 2050 utakuwa sehemu ya ajenda ya kudumu katika maamuzi na majukumu yenu ya kila siku.”

Alisema mipango, mikakati na utekelezaji wa taasisi za umma lazima viendane na malengo ya Dira 2050 ili kuchochea maendeleo ya Taifa.

"Mtakapotekeleza majukumu yenu kwa weledi, uwajibikaji na ufanisi, matokeo chanya yatapatikana na yatachangia kufanikisha maono ya Taifa," alisisitiza.

Aidha, aliwataka Watendaji Wakuu kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi ili kuongeza thamani ya huduma zinazotolewa na taasisi zao.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kujenga mifumo inayowawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, wawekezaji kupata huduma kwa wakati na taasisi za umma kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi.

Mhe. Kikwete pia alizitaka taasisi za umma kutumia mifumo ya kidijitali, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha utawala bora na kuhakikisha viashiria vya utendaji vinaakisi malengo ya Dira 2050.

Alieleza kuwa mafanikio ya mafunzo hayo hayatapimwa kwa idadi ya vyeti vilivyotolewa, bali kwa mabadiliko yatakayoonekana katika taasisi wanazoziongoza washiriki, ikiwemo utoaji bora wa huduma, matumizi yenye tija ya rasilimali za umma, ongezeko la mapato na uwajibikaji mkubwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Mipango na Uwekezaji anayeshughulikia Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo Tanzania imeingia katika kipindi muhimu cha mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kukuza uchumi wa Taifa hadi kufikia takribani mara kumi ya ukubwa wake wa sasa kupitia utekelezaji wa Dira 2050.

Alisema mazingira hayo yanahitaji viongozi wenye maono, ubunifu na uwajibikaji watakaoweza kutafsiri malengo ya kitaifa kuwa matokeo ya kiuchumi na kijamii yanayopimika.

"Nina imani kuwa maarifa mliyoyapata kupitia mafunzo haya pamoja na uzoefu mliobadilishana yatawaongezea uwezo na utayari wa kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi zaidi," alisema.

Aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha mageuzi makubwa ya uchumi, uongozi wenye maono, ubunifu na uwajibikaji utakuwa nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira 2050, akieleza kuwa taasisi za umma zina nafasi ya kipekee katika kuweka mazingira yatakayochochea uwekezaji, uzalishaji na ushindani wa uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake, Bw. Ibrahim Mahumi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, alisema kuimarisha uwezo wa uongozi wa Watendaji Wakuu ni msingi muhimu wa kuboresha ubora wa huduma za umma na kuhakikisha taasisi hizo zina uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Bw. Mahumi alisema viongozi hao wana wajibu wa kujenga utamaduni wa weledi, uwajibikaji na utendaji unaozingatia matokeo katika taasisi wanazoziongoza, akisisitiza kuwa uongozi madhubuti ni msingi wa kujenga taasisi zinazotoa huduma bora kwa wananchi.

Aliongeza kuwa maarifa na uzoefu walioupata washiriki kupitia mafunzo hayo yanapaswa kutafsiriwa kuwa hatua za vitendo kupitia kuboresha maamuzi ya kiutendaji, kuimarisha mifumo ya uongozi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Akitoa mtazamo wa taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema mageuzi yanayoendelea katika taasisi za umma tayari yameanza kuzaa matunda kupitia kuboreshwa kwa utoaji wa huduma, kuongezeka kwa ufanisi wa kiuchumi na kuimarika kwa utendaji wa taasisi nyingi za umma.

Kwa sasa, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia taasisi za umma na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache 308 zenye thamani ya uwekezaji wa Sh92.3 trilioni, hali inayozifanya kuwa mhimili muhimu katika utekelezaji wa Dira 2050 na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kutokana na nafasi hiyo, Bw. Mchechu alisema mageuzi yanayoendelea yanaonesha kuwa taasisi hizo zina uwezo wa kuwa injini muhimu ya ukuaji wa uchumi endapo zitaendelea kuongozwa kwa misingi ya uwajibikaji, ubunifu na usimamizi bora wa rasilimali.

“Katika miaka ya hivi karibuni, taasisi za umma zimepiga hatua kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa kiuchumi na kuimarisha utendaji wake kwa ujumla,” alisema.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yamewezesha baadhi ya taasisi kupunguza utegemezi wake kwa Mfuko Mkuu wa Serikali, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa uwezo wa kujitegemea kifedha na kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa.

"Tunaendelea kusukuma ajenda maalumu ya mageuzi ili, baada ya muda, taasisi nyingi zaidi ziweze kujiendesha kwa mapato yao wenyewe, isipokuwa zile ambazo kwa asili ya majukumu yake zinapaswa kuendelea kupata ruzuku ya Serikali," alisema.

Bw. Mchechu alisema mafanikio ya mageuzi hayo hayapaswi kupimwa kwa takwimu za kifedha pekee, bali pia kwa mabadiliko ya fikra, utamaduni wa utendaji na uwezo wa viongozi wa taasisi hizo kusimamia mabadiliko.

"Kwangu mimi mafanikio haya siyo suala la namba pekee; ni suala la mtazamo, fikra na utamaduni mpya tunaouona ndani ya Bodi zetu na kwa Watendaji Wakuu. Uwezo tunaouona ni mkubwa, kujitoa kwao ni kwa kiwango kingine, na kila mmoja anaonesha kiu ya mabadiliko na mafanikio," alisema.

Alisema dhamira hiyo imeongeza umiliki wa mageuzi miongoni mwa viongozi wa taasisi za umma na kuweka msingi imara wa kufanikisha Dira 2050 kupitia taasisi zenye ufanisi, zinazojitegemea zaidi kifedha na zinazotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024, Programu ya Mafunzo Elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma imewanufaisha takribani Watendaji Wakuu 244, ambapo viongozi 57 walishiriki katika awamu ya mwaka huu.

Programu hiyo huandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga viongozi wenye uwezo wa kuongoza taasisi za umma kwa ufanisi, kuimarisha utawala bora, kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha Dira 2050 inatafsiriwa kuwa matokeo halisi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com