Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa GCLA, Daniel Ndiyo akizungumza wakati akiwakaribisha wadau wakemikali aina ya Sulphur katika kikao cha wadau hao kilichofanyika katika ukumbiwa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.
******************
Na. Judith Meingarai
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewakutanisha wadau wa biashara na usafirishaji wa kemikali aina ya sulphur (salfa) kujadili mikakati ya kuboresha usafirishaji salama wa kemikali hiyo ili kupunguza ajali na kuifanya biashara hiyo kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuzingatia sheria na viwango vya usalama.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam Julai 24, 2026, Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa GCLA, Daniel Ndiyo, amesema Serikali imeamua kuwakutanisha wadau ili kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha usimamizi wa kemikali hiyo katika hatua zote za kuingia nchini, kuhifadhi na kusafirishwa.
Amesema sulphur ni miongoni mwa kemikali zinazopitishwa kwa wingi nchini kuelekea mataifa jirani kwa matumizi ya uchimbaji wa madini ya shaba (copper), hivyo biashara hiyo imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi pamoja na kuongeza shughuli za bandari na sekta ya usafirishaji.
"Tumekutana kama wadau kujadili namna bora ya kuboresha biashara hii, kutatua changamoto zilizopo na kuhakikisha usafirishaji wa sulphur unafanyika kwa usalama zaidi huku ukiendelea kuleta manufaa kwa uchumi wa nchi," amesema Ndiyo.
Amefafanua kuwa tangu Serikali iliporuhusu uingizaji wa sulphur mwaka 2019, na kuanza kuingia kupitia Bandari za Dar es Salaam na Tanga kuanzia Julai 2021, jumla ya meli 112 zimeingiza zaidi ya tani milioni 3.87 za kemikali hiyo.
Ameongeza kuwa, kiwango hicho ni sawa na takribani malori zaidi ya 129,000, hali inayochochea ajira kwa maelfu ya madereva, wasafirishaji, wahudumu wa mizigo na wadau wengine katika mnyororo mzima wa biashara.
Akizungumzia usalama wa usafirishaji, Ndiyo amesema takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2024 hadi 2026 kumekuwa na ajali 62 zilizohusisha usafirishaji wa sulphur, akisisitiza kuwa hata ajali moja ya kemikali inaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu, mazingira na miundombinu.
"Hatutaki kuanza na hatua za adhabu. Tunataka tujenge utaratibu kwa pamoja, tukubaliane kwa pamoja na kila mmoja awajibike kuhakikisha biashara hii inafanyika kwa usalama na inaendelea kuwa endelevu," alisema Ndiyo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Charles Ndyetabula, amesema elimu kwa wasafirishaji na udhibiti wa uzito wa mizigo ni maeneo muhimu yatakayosaidia kupunguza ajali.
Amesema takwimu za mwezi Mei hadi Julai mwaka huu wa 2026 kutoka Kituo cha Mizani cha Vigwaza zinaonesha kuwa kati ya malori 34 hadi 38 yalibainika kuzidisha uzito wa mizigo, hali inayoweza kuongeza hatari ya kumwagika kwa sulphur barabarani na kuhatarisha usalama wa wananchi.
Naye mwakilishi wa kampuni ya SAS Logistics, Sadick Simba, amesema pamoja na elimu ya usalama, ni muhimu kuhakikisha magari yanapata matengenezo ya mara kwa mara na madereva wanazingatia viwango vya mwendo vilivyowekwa ili kulinda maisha ya wananchi, mazingira na mali wakati wa usafirishaji wa kemikali.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau kutoka taasisi za Serikali, mamlaka za usimamizi na udhibiti, kampuni za uingizaji, uhifadhi na usafirishaji kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha usafirishaji wa sulphur nchini unakuwa salama na wenye ufanisi na endelevu.
Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda Mashariki, Danstan Mkapa, akiwasilisha mada kuhusu uhifadhi na usafirishaji wa kemikali aina ya Sulphur kwa wadau wa kemikali hiyo (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.
Meneja wa Ukaguzi wa kemikali na Maabara za Kemia, Gerald Meliyo, akizungumza wakati akimkaribisha Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, kufungua kikao cha wadau wa kemikali aina ya Sulphur kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.
Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Kati, Magdalena Mtenga, akieleza kuhusu mwenendo wa ajali za kemikali aina ya Sulphur katika eneo la Kanda ya Kati kwenye kikao cha wadau wa kemikali hiyo (hawapo pichani) kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.
Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima, akieleza kuhusu ajali za kemikali zilizotokea na namna ya kujikinga kwa wadau wa kemikali aina ya Sulphur (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.
Baadhi ya wadau wa kemikali aina ya Sulphur wakichangia mada mbalimbali katikakikao cha wadau kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.
Wadau wa kemikali aina ya Sulphur wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dar es Salaam Julai 24, 2026.







Social Plugin