Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imeanza kuzaa matunda katika sekta ya elimu baada ya Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) kutoa nafasi 10 za ufadhili wa masomo kwa Watanzania pamoja na kuimarishwa kwa ushirikiano wa kitaaluma kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema mafanikio hayo yametokana na mazungumzo yaliyofanyika wakati wa ziara ya Rais Samia nchini humo.
Alisema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni Rais Samia kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na RUDN, taasisi inayotambulika kimataifa kwa mchango wake katika elimu, tafiti na ubunifu wa kisayansi.
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, kutunukiwa kwa Rais Samia shahada hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa Tanzania na Urusi katika sekta ya elimu na kumefungua milango ya ushirikiano mpana zaidi kati ya taasisi za elimu za mataifa hayo.
“Chuo kilichomtunuku Rais Samia shahada kimetupa scholarship 10 tayari ili tuwe tunawapeleka Watanzania kwenda kusoma kule na kuwa na ushirikiano mbalimbali. Tunatamani kuona Watanzania wengi zaidi wanapata nafasi ya kwenda kusoma katika chuo hicho,” amesema.
Aidha, amesema Wizara ya Elimu ya Tanzania na Wizara ya Elimu ya Urusi zimesaini hati tatu za makubaliano zitakazowezesha kubadilishana walimu, wanafunzi na uzoefu wa kitaaluma pamoja na kuendeleza ufundishaji wa lugha za Kiswahili na Kirusi.
Prof. Mkenda amesema makubaliano hayo yataongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu nchini kwa kuwapa wataalamu na wanafunzi nafasi ya kujifunza mifumo mipya ya ufundishaji, tafiti na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Ameongeza kuwa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) nayo imesaini makubaliano mawili yatakayowezesha wanafunzi wa shahada ya kwanza na uzamili kusoma sehemu ya masomo yao Tanzania na sehemu nyingine nchini Urusi kabla ya kuhitimu.
Amesema mfumo huo wa masomo ya pamoja utawapa wanafunzi elimu yenye viwango vya kimataifa na vyeti vitakavyotambulika katika nchi zote mbili, hatua itakayoongeza ushindani wao katika soko la ajira.
Prof. Mkenda amesema Serikali pia inaendelea kukamilisha makubaliano ya utambuzi wa sifa za kitaaluma na vyeti vinavyotolewa na pande zote mbili ili kuondoa changamoto zinazowakabili wahitimu wanaotaka kujiunga na bodi mbalimbali za taaluma.
“Urusi ipo vizuri sana kwenye masuala ya elimu, hasa sayansi, teknolojia na uhandisi. Tungependa kuona Watanzania wengi zaidi wanatumia fursa hizi kwa sababu vyuo vyao vinaheshimika sana duniani,” amesema.
Amesema Serikali inapanga kutumia mfumo wa Samia Scholarship kupata wanafunzi watakaonufaika na nafasi hizo za masomo, huku wakipatiwa mafunzo ya lugha ya Kirusi nchini kabla ya kuanza masomo yao.
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika elimu ya juu nchini Urusi na kuwajengea uwezo katika sekta za sayansi, teknolojia, uhandisi na ubunifu ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.




Social Plugin