Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU AIELEZA ILO MAMBO SITA YANAYOIPAISHA TANZANIA KATIKA SEKTA YA KAZI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akizingumza katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani ( ILO), leo Juni 5, 2026, Jijini Geneva, Uswisi.

************

Na: OWM (KAM) - Geneva, Uswisi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amebainisha mambo sita makubwa ambayo Tanzania imeendelea kuyatekeleza katika kuimarisha sekta ya kazi, ajira na ustawi wa wafanyakazi, hatua zinazoiwezesha nchi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Mhe.Sangu ameyasema hayo Juni 5, 2026 Mjini Geneva, Uswisi katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unashirikisha wawakilishi wa Serikali, Waajiri na Wafanyakazi kutoka nchi wanachama 187.

Waziri Sangu ametaja mambo hayo ni pamoja na dhamira ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mabadiliko ya kiteknolojia yanakuza kazi zenye staha, tija, ubunifu na haki ya kijamii kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameeleza kuwa mageuzi hayo yameongeza ushiriki wa wanawake, vijana na wananchi wa vijijini katika huduma za kifedha na shughuli za kiuchumi huku Serikali Mtandao ikiimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa utoaji huduma.

Pia amesema Tanzania imeendelea kulinda haki za wafanyakazi katika mazingira ya kidijitali kupitia uzinduzi wa Mpango wa Taifa wa Kazi Zenye Staha (NDWCP III), pamoja na kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi kwa kutekeleza mpango wa Vision Zero na mifumo mingine ya ulinzi wa kazi.

Sangu ametaja jambo la tatu kuwa ni kuimarishwa kwa mifumo ya hifadhi ya jamii kupitia Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2023, ambapo zaidi ya wanachama 560,000 wa sekta isiyo rasmi na wanaojiajiri wamefikiwa kupitia usajili wa kidijitali kufikia Machi 2026.

Amesema jambo la nne ni kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa “e-UTATUZI” unaotumiwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ambao umeboresha usimamizi wa migogoro ya kazi kwa kurahisisha wafanyakazi na waajiri kufungua malalamiko na kuwasilisha mashauri mtandaoni kutoka sehemu yoyote nchini.

Jambo la tano ni kuimarishwa kwa mazungumzo ya kijamii ya pande tatu kupitia ushirikiano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi, hatua iliyowezesha kuwepo kwa kiwango cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi kuanzia Januari 1, 2026 pamoja na marekebisho ya sheria za kazi yaliyofanyika mwaka 2025.

Aidha, jambo la sita ni kuendelea kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika kuhakikisha matumizi ya Teknolojia ya Akili Bandia (AI) yanachochea maendeleo endelevu, ujumuishi, haki ya kijamii na ukuaji wa uchumi unaowanufaisha wananchi wote.

Mhe. Sangu amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa kazi wa ndani na wa kimataifa ili kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanatumika kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza tija na kuimarisha ustawi wa wafanyakazi nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akizingumza katika Mkutano Mkuu wa 114 wa Shirika la Kazi Duniani ( ILO), leo Juni 5, 2026, Jijini Geneva, Uswisi.
Sehemu ya Ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) katika Mkutano Mkuu wa 114 wa ILO unaofanyika Jijini Geneva, Uswisi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akipongezwa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa Nchini Uswisi, Mhe. Dkt. Abdallah Possi mara baada ya kutoa tamko la Serikali ya Janhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), leo Juni 5, 2026, Jijini Geneva, Uswisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com