Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAPATO YA NDANI YAENDELEA KUWA NGUZO YA MIRADI YA MAENDELEO



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Serikali imesema itaendelea kutegemea mapato ya ndani kama chanzo kikuu cha kugharamia matumizi yake na kutekeleza miradi ya maendeleo, ikieleza kuwa mafanikio ya ukusanyaji wa kodi na mapato mengine yameiwezesha kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kabla ya kuwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni.

Alisema ongezeko la mapato ya ndani limeiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za matumizi katika mwaka wa fedha unaomalizika.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, bajeti ya mwaka 2026/2027 ni ya kihistoria kwa kuwa ndiyo ya kwanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa 2026/27 hadi 2030/31 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025.

Alisema Serikali itaendelea kuelekeza rasilimali katika miradi ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa mtandao wa barabara, miradi ya maji na nishati pamoja na uwekezaji katika maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi.

Balozi Omar alisema maandalizi ya bajeti yamezingatia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ambapo jumla ya mapendekezo 727 yalipokelewa kutoka kwa wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu pamoja na wananchi mmoja mmoja.

Alieleza kuwa baada ya uchambuzi wa Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi, mapendekezo 125 yalikubaliwa kama yalivyowasilishwa, 121 yakafanyiwa maboresho kabla ya kukubaliwa, huku 295 yakikataliwa na mengine kuendelea kufanyiwa tathmini au kupelekwa katika taasisi husika kwa uchambuzi zaidi.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha kila shilingi inayokusanywa inaleta matokeo chanya kwa maendeleo ya wananchi.

Aliwataka Watanzania kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati pamoja na kufuatilia hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 ili kuelewa vipaumbele na mwelekeo wa uchumi wa taifa katika mwaka mpya wa fedha.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com