Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LIGI YA MAJI CUP 2026 YAANZA KUTIMUA VUMBI CCM KAMBARAGE - SHINYANGA


Na Michael Abel, Shinyanga.

Ligi ya Maji Cup 2026 Kanda ya Ziwa imeanza rasmi kutimua vumbi katika Uwanja wa CCM Kambarage uliopo Manispaa ya Shinyanga, ikiwakutanisha watumishi wa mamlaka mbalimbali za maji pamoja na timu za wadau wa jamii zikiwemo za waendesha bodaboda.

Mashindano hayo yameanza leo Juni 05, 2026, yanahusisha timu za mamlaka za maji kutoka kanda ya Ziwa katika mikoa 3 ya Shinyanga, Mara na Simiyu, huku timu nne bora zikitarajiwa kufuzu kushiriki fainali za kitaifa zitakazofanyika jijini Mwanza, nyenye Kaulimbiu inasema, “Kuongeza Kasi ya Utekelezaji wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Kupunguza Upotevu wa Maji kwa Huduma Endelevu.”

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mtendaji Mkuu wa ATAWAS, Costantino Chiwaligo, ambaye pia ni Mratibu wa mashindano hayo, amesema lengo kuu la Ligi ya Maji Cup ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji, miundombinu ya maji na mazingira kupitia michezo. Alieleza kuwa mashindano hayo yanatumika kama jukwaa la kuisogeza jamii karibu na mamlaka za maji ili kufikisha ujumbe wa uhifadhi wa rasilimali za maji.

Chiwaligo amesema mbali na timu za mpira wa miguu, mashindano hayo pia yanashirikisha timu za mpira wa pete na baadhi ya timu za jamii ili kuongeza wigo wa ushiriki wa wananchi. Amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea wananchi uelewa na kuwafanya kuwa mabalozi wazuri wa kulinda vyanzo vya maji, kuzuia uharibifu wa miundombinu ya maji na kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, ambaye ni mwenyeji wa mashindano hayo, amewataka wachezaji wote kushiriki kwa nidhamu na weledi huku wakizingatia maadili na miiko ya utumishi wa umma huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa mamlaka za maji.

Akifungua rasmi mashindano hayo, Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Pendo Sawa, amewataka watumishi wa mamlaka za maji kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti upotevu wa maji na kuimarisha huduma kwa wananchi huku akihimiza jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji dhidi ya uharibifu na hujuma.

Katika mashindano hayo siku ya leo timu ya mpira wa miguu ya SHUWASA imeifunga timu ya RUWASA Shinyanga goli 2 - 0 huku timu ya RUWASA Mwanuzi ikiichakaza goli 6 - 0 RUWASA Mara na SHUWASA ikitoka sare ya 1 - 1 dhidi ya timu ya Bodaboda. huku timu ya mpira wa pete ya SHUWASA ikiifunga goli 37-17 RUWASA Shinyanga.

<<<<Tazama Picha>>>>


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza kwenye mashindano hayo.

Mtendaji Mkuu wa ATAWAS, Costantino Chiwaligo, ambaye pia ni Mratibu wa mashindano akizungumza kwenye mashindano hayo.

Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Pendo Sawa akizungumza kwenye mashindano hayo.

































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com