Na Bora Mustafa, Arusha
Wanawake wa Afrika Mashariki wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, ubunifu na akili mnemba (AI) ili wawe sehemu ya viongozi wa mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea duniani na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kanda hiyo.
Wito huo umetolewa Juni 25, 2026 na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakati wa mjadala uliojadili nafasi ya wanawake katika kuongoza mustakabali wa kidijitali wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), George Odong amesema mjadala huo umefanyika katika kipindi muhimu ambapo teknolojia za kidijitali, ubunifu na akili mnemba vinaendelea kubadilisha namna watu wanavyoishi, kufanya kazi na kuwasiliana.
Amesema jukumu la Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuhakikisha mustakabali wa kidijitali wa kanda hiyo unakuwa jumuishi, wenye usawa na unaozingatia matarajio ya wananchi wote.
Aidha, amesema EALA itaendelea kuhakikisha sauti za wanawake, vijana, asasi za kiraia na sekta binafsi zinazingatiwa katika mchakato wa kufanya maamuzi ya kikanda ili kuimarisha maendeleo ya pamoja.
Kwa upande wake, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika Mashariki, Rebecca Kadaga, amesema wanawake wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mifumo ya kifedha ya kidijitali na majukwaa ya ubunifu ili kuunganisha mawazo yao na wawekezaji, kupanua mitandao ya ushauri na kuongeza fursa za maendeleo barani Afrika.
Kadaga pia amesisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa kidijitali na usawa wa kijinsia katika elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akitaka kuongezwa kwa ufadhili wa masomo, udhamini na ulinzi wa kisheria ili kukuza usawa wa kijinsia na kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata mazingira salama ya kutumia teknolojia.
Naye Katibu Mkuu wa EAC, Steven Patrick Mbundi, amesema wanawake wa Afrika Mashariki katika vizazi vyote hawapaswi tena kusubiri kualikwa kwenye meza za maamuzi, bali wanapaswa kujenga meza zao wenyewe kupitia uongozi, ubunifu na ushirikiano.
“Wanawake wana nafasi kubwa ya kuongoza mabadiliko ya kidijitali yanayoendelea duniani, hivyo ni muhimu kuweka mazingira yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa maarifa na teknolojia,” amesema Mbundi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake la EAC, Fatuma Ndangiza, amesema kuongoza mustakabali wa kidijitali kunamaanisha kuwaweka wanawake mstari wa mbele katika uchumi wa kanda, hususan wafanyabiashara wa mipakani, wajasiriamali na kampuni zinazoongozwa na wanawake.
Amesema hatua hiyo itawawezesha wanawake kunufaika zaidi na fursa za biashara, uwekezaji na masoko mapya yanayotokana na maendeleo ya teknolojia na ushirikiano wa kikanda.
Ndangiza amesema muongo ujao hautakuwa wa teknolojia za kidijitali pekee, bali pia wa akili mnemba, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya mchakato huo ili wasibaki nyuma katika mapinduzi mapya ya kiteknolojia.



Social Plugin