Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude
Na Bora Mustafa, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema jumla ya watuhumiwa 413 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, huku akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya tatizo hilo yanahitaji ushiriki wa wananchi na wadau mbalimbali.
Mkude ametoa kauli hiyo Juni 25, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika Kanisa la Selian Community Church jijini Arusha.
Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Ubunifu wa Kimkakati: Suluhisho la Changamoto za Dawa za Kulevya."
Amesema maadhimisho hayo yanatoa nafasi kwa jamii kutafakari kwa pamoja athari za dawa za kulevya na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo linaendelea kuhatarisha afya, amani na maendeleo ya jamii.
"Dawa za kulevya ni adui wa amani yetu, adui wa familia zetu na adui wa mustakabali wa watoto wetu," amesema Mkude.
Akieleza mafanikio ya operesheni zilizotekelezwa wilayani Arusha kati ya Julai 2025 na Juni 2026, Mkude amesema watuhumiwa 413 walikamatwa, wakiwemo wanaume 338 na wanawake 75. Aidha, kilo 1,458.26 za mirungi na kilo 2,977.03 za bangi zilikamatwa katika operesheni hizo.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya DCEA, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wanaoendelea kutoa taarifa zinazowezesha kubaini na kukamata wahusika wa biashara hiyo haramu.
Hata hivyo, Mkude amesema bado kuna changamoto katika vita dhidi ya dawa za kulevya kutokana na Mkoa wa Arusha kuwa kitovu cha biashara, utalii na mikutano ya kimataifa, hali inayoweza kuvutia mitandao ya biashara haramu ya dawa hizo.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kuachiwa serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wazazi, viongozi wa dini, taasisi za elimu, viongozi wa jamii na wananchi wote. Pia ametoa wito wa kuwekeza zaidi katika elimu, malezi bora na maadili kwa vijana ili kuzuia matumizi ya dawa za kulevya kabla hayajaleta madhara makubwa kwa jamii.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Brenda Mbati, akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo, amesema jumla ya watuhumiwa 550 walikamatwa katika operesheni 227 zilizofanyika katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara katika kipindi hicho.
Amesema kati ya watuhumiwa hao, wanaume walikuwa 442 na wanawake 108. Aidha, kilo 5,417.26 za mirungi, kilo 3,010.30 za bangi pamoja na gramu 14 za heroin zilikamatwa katika operesheni mbalimbali zilizotekelezwa ndani ya mwaka mmoja.
Brenda amesema Mkoa wa Arusha uliongoza kwa idadi ya operesheni kwa kutekeleza operesheni 121 na kukamata watuhumiwa 413, ukifuatiwa na Mkoa wa Kilimanjaro ambao ulifanya operesheni 50 na kukamata watuhumiwa 72.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkoa wa Tanga ulitekeleza operesheni 49 zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 33 pamoja na kilo 1,814.49 za mirungi, kilo 20.25 za bangi na gramu 14 za heroin. Pia, pikipiki 50 zilizokuwa zikitumika kusafirisha mirungi zilikamatwa na watuhumiwa 19 kuhusishwa na matukio hayo.
Katika Mkoa wa Manyara, operesheni saba zilifanyika na kusababisha kukamatwa kwa watuhumiwa 32 pamoja na kilo 575.90 za mirungi.
Brenda amesema hatua za kisheria zimeendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa biashara ya dawa za kulevya, ambapo watuhumiwa 10 walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela katika kesi mbalimbali, huku wengine wakipewa adhabu tofauti kulingana na makosa yao.
Aidha, amesema wananchi 136,132 walifikishwa na kupewa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji zilizofanyika katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Katika huduma za matibabu na urejeshaji wa waraibu, amesema DCEA inaendelea kushirikiana na nyumba 32 za upataji nafuu zinazohudumia waraibu 937. Vilevile, vituo vya tiba mbadala ya utegemezi wa dawa za kulevya vimetoa huduma kwa wagonjwa 771, huku watu 325 wakifanikiwa kumaliza matibabu yao.
Brenda amesema maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu ya "Ubunifu wa Kimkakati: Suluhisho la Changamoto za Dawa za Kulevya," yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya mbinu mpya, ushirikiano wa wadau na ubunifu katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na DCEA pamoja na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya ili kuimarisha usalama wa jamii na kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya athari za matumizi na biashara haramu ya dawa hizo.


Social Plugin