Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAIELEZEA DUNIA HATUA ZILIZOPIGWA KATIKA KULINDA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU


Na Mwandishi wetu-New York, Marekani.


Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameieleza Jumuiya ya Kimataifa hatua kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kulinda na kuendeleza haki za watu wenye ulemavu, wakati aliposhiriki Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19) unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani.

Mhe. Mahundi, ambaye amemuwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Palamagamba John Kabudi, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kiutendaji ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki, fursa na huduma stahiki kama wananchi wengine.

Akiwasilisha taarifa ya nchi, Mhe. Mahundi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 kwa Tanzania Bara pamoja na Sheria Na. 8 ya mwaka 2022 ya Zanzibar, ambazo zimeweka msingi imara wa kulinda haki na ustawi wa watu wenye ulemavu.

“Masuala ya ulemavu yamejumuishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mipango mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo ya taifa na kusema kuwa Serikali imeendelea kupanua upatikanaji wa elimu jumuishi, huduma za afya, huduma za urekebishaji na tiba, teknolojia saidizi, programu za uwezeshaji kiuchumi pamoja na huduma za hifadhi ya jamii kwa watu wenye ulemavu” amesema Mhe. Mahundi.

Aidha Mhe. Mahundi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake madhubuti na dhamira ya dhati ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma bora na fursa zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

“Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama, Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia na watu wenye ulemavu wenyewe katika kuharakisha utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu na kujenga jamii jumuishi inayoheshimu usawa, utu na haki za kila mtu,” amesema Mhe. Mahundi.

Mkutano huo wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu umebeba kaulimbiu inayosema “CRPD at 20: Celebrating and Consolidating Achievements and Shaping the Next Phase of Implementation in a Changing World,” ukilenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mkataba huo na kuweka mikakati ya kuendeleza utekelezaji wake duniani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com