Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Mhe. David Kafulila, amesema Tanzania inahitaji kuongeza kasi ya maendeleo kuliko ilivyofanya Singapore ili kufikia lengo la kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Kafulila ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, akieleza kuwa ziara ya Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, pamoja na mhadhara wake Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) imeibua hamasa kubwa miongoni mwa viongozi wa serikali, wanazuoni, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuhusu safari ya maendeleo ya Singapore kutoka taifa la kipato cha chini hadi kuwa miongoni mwa mataifa yenye maisha bora zaidi duniani.
Akinukuu takwimu za IMF za mwaka 2026, Kafulila amesema Singapore ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa pato la mtu mmoja mmoja, likifikia zaidi ya dola 107,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, amesema kuwa licha ya mafanikio hayo, uchumi wa Singapore bado haujafikia dola trilioni moja, ukiwa na thamani ya takribani dola bilioni 659.
Kafulila ameeleza kuwa mwaka 1995 uchumi wa Singapore ulikuwa karibu sawa na wa Tanzania, ukiwa katika kiwango cha dola bilioni 87, jambo linaloonyesha kuwa Tanzania inapaswa kuongeza kasi zaidi ya ile iliyotumiwa na Singapore ili kufikia lengo la uchumi wa dola trilioni moja mwaka 2050.
Amesema mafanikio hayo yanahitaji mabadiliko makubwa katika namna ya kufanya kazi na kusimamia maendeleo, akirejea kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwamba ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inapaswa kubadilika kwa kiwango kikubwa zaidi katika mifumo na mbinu za utekelezaji.
Wakati huo huo, Rais Tharman Shanmugaratnam amesisitiza umuhimu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), akizitaka serikali za Afrika kuacha kuendesha miradi ambayo inaweza kufanywa kwa ufanisi zaidi na sekta binafsi.
Amesema hatua hiyo itaziwezesha serikali kuelekeza rasilimali zake katika maendeleo ya watu kupitia elimu, afya na ujuzi.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa Singapore, ubora wa rasilimali watu ndio msingi wa ushindani wa taifa lolote duniani, huku akibainisha kuwa maendeleo ya watu ndiyo yanayoamua nchi kuwa mstari wa mbele au kubaki nyuma katika uchumi wa dunia.

Social Plugin