
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali imefikia hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya madini baada ya kuridhia kutenga asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na sekta hiyo kwa ajili ya kugharamia utafiti wa kina wa rasilimali za madini nchini.
Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 22, 2026, Mavunde amesema hatua hiyo ni ya kihistoria na itawezesha Tanzania kuongeza uelewa wa kina kuhusu utajiri wa madini uliopo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika shughuli za utafiti wa jiolojia ambapo hadi sasa imefanya geological mapping kwa asilimia 97, geochemical survey kwa asilimia 24 na low resolution survey kwa asilimia 100 tangu tafiti hizo zilipoanza kufanyika katika miaka ya 1978 na 1979.
Hata hivyo, Mavunde amebainisha kuwa maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya sekta ya madini yanahitaji utafiti wa kina zaidi unaojulikana kama high resolution survey ili kubaini kwa usahihi maeneo yenye viashiria vya madini na mipasuko ya miamba inayobeba rasilimali hizo.
Amssema licha ya Tanzania kuwa na eneo la kilometa za mraba 945,000, utafiti huo wa kina umefanyika katika asilimia 16 pekee ya eneo lote la nchi, huku asilimia 84 iliyobaki ikiwa bado haijafanyiwa uchunguzi wa kiwango hicho.
“Leo nasimama hapa kusema kwamba katika historia ya nchi yetu tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini miaka 101 iliyopita, ndani ya miaka michache ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan historia mpya inaandikwa,” alisema Mavunde.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Bajeti Kuu ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Serikali imeridhia kutenga asilimia 10 ya mapato yanayotokana na sekta ya madini kwa ajili ya kuimarisha shughuli za utafiti wa kina wa madini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, uamuzi huo utatoa msukumo mkubwa katika kubaini maeneo mapya yenye utajiri wa madini, kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta hiyo na kuongeza mchango wa madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mavunde amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza sekta ya madini na kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zake za asili kupitia tafiti za kisasa na za kina.




Social Plugin