Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. MWAFISI ASISITIZA UANDISHI WA KIZALENDO KULINDA MASLAHI YA TAIFA NA KUEPUKA MKUMBO WA KUBOMOA AMANI


Na Mwandishi Wetu

Mwanahabari Mkongwe na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Dk Samwilu Mwafisi, ametoa mwito kwa wanahabari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuzingatia uandishi wenye kulinda maslahi ya taifa, huku akionya dhidi ya kufuata mikumbo inayoweza kuchochea uvunjifu wa amani na kuichoma nchi moto.

Akizungumzia wajibu wa tasnia hiyo, Dk Mwafisi alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuunda mtazamo wa jamii, ambapo vinaweza kujenga au kubomoa taswira ya nchi, hivyo uzalendo na maadili yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya kukimbilia faida za kifedha au umaarufu wa muda mfupi.

Alibainisha kuwa mabadiliko ya TEHAMA yameleta changamoto ya watu kusambaza habari potofu na za kusisimua bila uhakiki, jambo linalotumiwa na watu wenye nia ovu kushawishi jamii kufuata mikumbo ya kuvunja sheria, hususan wakati wa migogoro ambapo maslahi na usalama wa taifa lazima vipewe kipaumbele ili kulinda wananchi.

Dk Mwafisi alihitimisha kwa kusitiza kauli yake ya kutoficha changamoto bali kusema ukweli kwa weledi, akitoa rai kwa kila mwenye simu, kamera na kalamu kutoitumia kama silaha ya kujichafua au kuhatarisha amani, bali kuwa daraja thabiti la maendeleo na mshikamano kwa maslahi mapana ya nchi. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com