Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUWASA YAPOKEA MAONI YA WADAU KUUNDA DIRA YA MIAKA MITANO, TEKNOLOJIA NA UPANUZI WA HUDUMA VYAJITOKEZA


Kaimu Mkurugenzi wa KUWASA, Adam Mgongwa, akiwa katika mkutano wa wadau wa sekta ya maji uliofanyika Manispaa ya Kahama kwa ajili ya kukusanya maoni yatakayosaidia kuandaa Dira ya Maendeleo ya Miaka Mitano ya mwaka 2026 hadi 2031.

Na Neema Nkumbi, Kahama

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama mkoani Shinyanga (KUWASA) imekutana na wadau wa sekta ya maji kwa ajili ya kukusanya maoni yatakayosaidia kuandaa Dira ya Maendeleo ya Miaka Mitano ya mwaka 2026 hadi 2031, huku masuala ya matumizi ya teknolojia, upanuzi wa huduma za maji na uboreshaji wa huduma kwa wateja yakipewa kipaumbele.


Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa KUWASA, Adam Mgongwa, amesema taasisi hiyo imeendelea kuboresha mifumo ya kidigitali ili kurahisisha huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za maji.

Amesema KUWASA imeondokana na mfumo wa bili za karatasi na sasa wateja hupokea taarifa za matumizi na bili zao kupitia ujumbe mfupi wa simu, huku malipo yakifanyika kupitia mifumo mbalimbali ya kifedha bila kulazimika kufika ofisini.


"Tulianza na bili za karatasi ambazo ilikuwa lazima mteja akabidhiwe kwa mkono, lakini sasa tumetoka huko, Wateja wanapata bili kupitia simu zao na wanaweza kulipa popote walipo pia maombi ya kuunganishiwa huduma mpya yanafanyika kwa njia ya mtandao bila mteja kufika ofisini," amesema Mgongwa.
Kwa upande wake, Afisa Mahusiano kwa Umma wa KUWASA, John Mkama, amesema utoaji wa huduma bora ni msingi wa kuongeza imani ya wateja na kuwahamasisha kulipa bili zao kwa wakati.


Amesema wananchi wanapaswa kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya maji kwani mara nyingi bili kubwa husababishwa na matumizi yasiyodhibitiwa katika kaya, huku ukaguzi unaofanywa ukionyesha kuwa mita nyingi za maji hufanya kazi kwa usahihi.


"Mteja anaporidhika na huduma anayoipata huwa tayari kulipa bili yake, Tunapaswa kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya maji na kuhakikisha changamoto zinazoripotiwa na wananchi zinatatuliwa kwa wakati," amesema Mkama.


Naye mdau wa maji, Wisaka Kamwamu, amependekeza kuongezwa kwa matumizi ya mita za kidigitali akisema mfumo huo utasaidia kupunguza malalamiko yanayotokana na makadirio ya matumizi ya maji na bili zinazolalamikiwa na baadhi ya wananchi.


"Changamoto kubwa tunayokutana nayo mara nyingi ni malalamiko kuhusu bili, Mita za kidigitali zitasaidia wananchi kuona matumizi yao halisi na kupunguza migogoro inayotokana na makadirio," amesema Kamwamu.

Kwa upande mwingine, Andason Lyimo amewataka wataalamu wa maji kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mita zilizofungwa kwa wateja ili kubaini mapema hitilafu zinazoweza kuathiri usomaji sahihi wa matumizi ya maji.


Amesema baadhi ya mita zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu hivyo zinahitaji kufanyiwa tathmini ili kuhakikisha zinaendelea kutoa taarifa sahihi za matumizi.


Katika maoni yake, Elizabeth Cosmas amesisitiza umuhimu wa kudhibiti uchafuzi wa maji na kuharakisha matengenezo ya mabomba yanayopasuka mara kwa mara, akieleza kuwa baadhi ya vitendo vya uchafuzi vinafanywa na watu wanaofahamu athari zake lakini hawachukuliwi hatua stahiki.

"Wanaosababisha uchafuzi wa maji wanapaswa kutambuliwa na kuchukuliwa hatua ili kulinda ubora wa huduma za maji kwa wananchi," amesema Cosmas.


Naye Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila, ameiomba KUWASA kutafuta fedha zaidi kupitia Serikali na wadau wa maendeleo ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Mji wa Kahama ambao unaongeza mahitaji ya huduma za maji kila mwaka.


Ametaja maeneo ya Nyahanga, Mlimani, Nzagamba, Kitwana na Nyamela kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuongezewa huduma ya maji, huku akisisitiza matumizi ya mabomba makubwa katika miradi mipya ili kuepusha gharama za kubadilisha miundombinu baada ya muda mfupi.

"Kahama inakua kwa kasi kubwa, Tunahitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika miradi ya maji na matumizi ya mabomba yenye uwezo wa kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye," amesema Simbila.


Wadau walioshiriki kikao hicho walikubaliana kuwa matumizi ya teknolojia, uboreshaji wa huduma kwa wateja, uhifadhi wa vyanzo vya maji, upanuzi wa miundombinu na ushirikishwaji wa wananchi ni miongoni mwa maeneo yatakayosaidia kuboresha huduma za maji katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Maoni hayo yanatarajiwa kuingizwa katika rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Miaka Mitano ya KUWASA ya 2026–2031, ambayo itakuwa mwongozo wa utekelezaji wa miradi na maboresho ya huduma za maji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com