Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJUZI NI AJIRA : HADITHI YA MAFANIKIO YA MIAKA 98 YA UANAGENZI PERAMIHO


Na Mwandishi Maalumu

Katika zama hizi za mapinduzi ya viwanda na soko shindani la ajira, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetambua umuhimu wa Chuo Chuo cha Ufundi Peramiho.

Kupitia Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi kwa njia ya Uanagenzi, serikali imewekeza rasilimali fedha kugharamia mafunzo kwa vijana wa Kitanzania 125. Huu si tu uwekezaji katika elimu, bali ni mkakati wa makusudi wa kuipunguzia mzigo nguvukazi iliyo mitaani bila ujuzi stahiki.

Kupelekwa kwa wanafunzi kwa gharama za serikali katika Chuo hiki kilichopo katika viunga vya Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, chenye kuta ambazo zimesimama imara kwa takriban karne moja sasa, sio tu kunahitimisha ukweli usemao ‘Ujuzi ni mali isiyopotea’ lakini wanafunzi wenyewe wanathibitisha kuendelea kwa ukuzaji na uimarishaji wa mwelekeo uliokuwa wazi: wakati kinaanzishwa chuo hiki 28 Juni1928, kugeuza nguvu ya ujana kuwa nguvu ya uzalishaji.

Ukitazama historia ya Chuo cha Ufundi Peramiho, kilichoanzishwa na wamisionari kutoka Ujerumani, kikiwa na miaka 98 sasa kimebaki kuwa mnara wa umahiri na chemchemi ya matumaini kikishuhudia mabadiliko ya nyakati huku kikibaki imara katika kutoa stadi zinazowajengea vijana wa Kitanzania uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.

Ushirikiano wa Kimkakati , Mbegu ya Uanagenzi Inavyochipua

Uso wa tabasamu wa Mkuu wa Chuo hicho, Frt. Martin Mrope, wakati wa mahojiano ulieleza pasi shaka matumaini ya kuendelea kwa chuo hicho kuwa wafuaji wa vijana katika bunifu mbalimbali ambazo zinawaweka kuwa mahiri katika shughuli zao za ufundi na stadi mbalimbali.

Akiweka wazi mafanikio ya sasa, Frt. Mrope alibainisha kuwa katika Awamu ya Nane ya utekelezaji wa Programu ya Ukuzaji Ujuzi kwa njia ya Uanagenzi, walipokea vijana 125 wenye shauku. Kati yao, vijana 118 wanaendelea vyema na masomo, wakichukua fani tano muhimu ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi wa maisha: Ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, Ufundi bomba (Plumbing), Useremala, Ufundi magari (Auto-mechanics), na Ufundi umeme wa majumbani.
Mafunzo haya si ya kukaa darasani kwa miaka mingi bila tija,ni mafunzo ya muda mfupi ya miezi minane—miezi sita ya kwanza ya nadharia na vitendo darasani, ikifuatiwa na miezi miwili ya vitendo kazini (field).

Frt. Mrope anafafanua kuwa lengo ni kumpa kijana stadi tatu kuu: ujuzi wa kujitegemea, uwezo wa kazi za mikono, na misingi ya ujasiriamali ili waweze kuanzisha shughuli zao za uzalishaji mali.

“Ndani ya miezi minane tu, vijana hawa wanabadilishwa kuwa wataalamu wa Ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, Ufundi bomba, Useremala, Ufundi magari, na Ufundi umeme wa majumbani” anasema Frt. Mrope huku akifafanua kwamba ujuzi huo si tu kwa ajili ya kuajiriwa, bali ni ufunguo wa ujasiriamali na kujitegemea.

Ushuhuda wa Wanagenzi

Januari Mwakilambo (19), anayejifunza fani ya ufundi bomba, anasema, “Kati ya miezi sita ya darasani, sasa naweza kufanya kazi ndogo ndogo za ufundi ikiwemo kuchora mfumo wa maji ndani ya nyumba.”

Shakira Sinakara (20), mwanafunzi wa fani ya ufundi bomba, aliongeza, “Vijiji vinakosa huduma ya maji kutokana na uchache wa mafundi. Pia fani hii ina wanawake wachache, hivyo nikaamua kuja kujifunza hapa Peramiho.”

Kwa upande wake Ali Hamis Kaukuya mwanagenzi fani ya umeme wa majumbani alisema mafunzo hayo yamewajengea stadi za maadili na umuhimu wa uaminifu kwenye kazi za ufundi.

“Ninajiona niko tofauti na nilivyotoka nyumbani. Uaminifu na siri ni silaha muhimu kwa kazi ya ufundi” na kuongeza kuwa somo la maadili limewafundisha kuwa kwenye nyumba za wateja wataona vitu vingi lakini hawapaswi kuvieleza hadharani alisema Kaukuya ambaye pia ni Rais wa wanagenzi chuoni hapo.
Mwanagenzi David Mapunda toka kijijini cha Namihoro akitoa maelezo kuhusu walichojifunza kwenye kozi ya ufundi bomba alionesha umahiri wa kueleza kwa mapana misingi ya kazi hiyo.

Kijana Mapunda alisema aliona tangazo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mafunzo ya uanagenzi na kuamua kwenda Chuo Peramiho kuchukua fomu kisha kutuma maombi.Mapunda anaishukuru Serikali kwa kugharimia mafunzo hayo yanaomhakikisha ujuzi mara baada ya kumaliza miezi nane ya mafunzo Septemba mwaka huu.

Wakufunzi wa Wanagenzi wanasemaje?

Dastan Komba, Mkufunzi wa fani ya umeme wa majumbani, anasema, “Programu ya uanagenzi ni muhimu kutokana na kusaidia vijana wasio na uwezo wa kujigharimia kupata fursa ya kusoma kwa gharama za Serikali.”

Sista Deogratia Mauki, Mkufunzi wa fani ya umeme, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwasaidia wasichana kupata nafasi za mafunzo ya ufundi. Kwenye darasa la umeme wa majumbani lenye wanagenzi 26 kati yao watano ni wasichana.

Sista Mauki alieleza umuhimu wa wasichana kujiunga na fani za ufundi kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ujuzi utakaowafanya wajiajiri mahala popote na kupunguza utegemezi kwa wenza wao.

“Tupewe nafasi kama mimi nimesoma Uhandisi Umeme (Electrical Engineering) chuo cha Ufundi Arusha na kuhitimu mwaka 2008 leo nafundisha vijana ufundi.Nimeona manufaa ya ufundi kwenye eneo letu, vijana wanajiajiri na wengine wamefungua maduka ya vifaa vya umeme vijijini” alisisitiza Sista Mauki.

Dira ya Taifa na Ahadi ya Kesho

Simulizi hii ya Peramiho ni sehemu ndogo ya picha kubwa ya Taifa. Aprili 2, 2026, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliwaambia Watanzania kuwa vijana 5,746 wananufaika na programu hii katika vyuo 46 nchini kote.

Dkt. Nchemba alibainisha kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana wa kitanzania kupata ujuzi kwa mafunzo ya muda mfupi wa miezi sita darasani na miezi miwili kwa vitendo hatua itayowasaidia kupata sifa stahiki za kujiajili na au kuajiliwa baada ya mafunzo.

Serikali inatekeleza Programu hiyo ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano .

Akizindua mafunzo ya Uanagenzi kwa mwaka 2025/26 tarehe 03 Machi 2026 jijini Dodoma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu, alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/26 Serikali imewezesha jumla ya vijana 5,746 kati yao vijana wa kiume ni 3,355 na wa kike ni 2,391 kupitia vyuo 46 vilivyopo katika mikoa 25.

Sangu alibainisha kuwa kati ya vyuo hivyo vyuo 29 ni vya Serikali na vyuo 17 ni vya binafsi na kwamba wapo vijana wenye Ulemavu ni 60, kati yao vijana 37 ni wa kiume na 23 ni wa Kike.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji vitendea kazi kwa wanagenzi wahitimu, Waziri Sangu alisema Serikali imetenga shilingi Bilioni moja katika bajeti ya mwaka 2026/27 kwa ajili ya kugharimia upatikanaji wa vifaa kwa vijana watakaohitimu mafunzo ya uanagenzi ili kuwaandaa kwenda kujiajiri.

Makala imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Ajira na Mahusiano

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com