NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema katika kipindi cha miaka 50 Shirika hilo limefanikiwa kujenga na kusimamia mifumo ya udhibiti ubora na usalama wa bidhaa nchini hatua iliyosaidia kuongeza tija katika uchumi na sekta ya Viwanda na Biashara kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Mei 15, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema TBS imeendelea kuwa taasisi muhimu katika kulinda afya na usalama wa walaji pamoja na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.
Amesema kadri uchumi wa Tanzania ulivyokuwa na mahitaji ya soko kubadilika, shirika hilo limepanua wigo wa huduma zake na kuwa mhimili muhimu katika sekta za viwanda, biashara na maendeleo ya uchumi.
Kwa mujibu wa Dkt. Katunzi, TBS imepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, kuongeza umahiri wa maabara, kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kuongeza utambulisho wa kimataifa katika masuala ya viwango.
Amesema mafanikio hayo yamechangia kutimiza azma ya Serikali ya kuwezesha biashara kwa kuwasaidia wazalishaji wa ndani kufikia masoko ya kikanda na kimataifa kupitia bidhaa zinazozingatia viwango vya ubora.
“Miaka 50 ni hatua kubwa inayostahili heshima, lakini pia ni nafasi ya kujitathmini na kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya shirika,” amesema.
Aidha, amesema maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya TBS yataambatana na uzinduzi wa kitabu maalum kitakachoeleza historia ya shirika hilo, mafanikio yaliyopatikana pamoja na mchango wake katika maendeleo ya taifa kwa kipindi chote cha miaka 50.
Dkt. Katunzi amesema TBS imeandaa matukio mbalimbali ya kuadhimisha jubilei hiyo, ikiwemo Viwango Marathon itakayofanyika Mei 23, 2026 katika Viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.
Pia kutafanyika Jukwaa la Biashara la Viwango (Viwango Business Forum) Juni 5, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, litakalowakutanisha wenye viwanda, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wataalamu wa viwango kujadili namna viwango vinavyoweza kukuza biashara.
Kwa upande mwingine, TBS itaandaa Usiku wa Jubilei ya Dhahabu (Gala Dinner) kwa ajili ya kutoa shukrani kwa watumishi waliostaafu na waliopo kazini waliotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya shirika hilo.
Shirika hilo pia linatekeleza jukumu la kurudisha kwa jamii kupitia utoaji wa msaada kwa hospitali yenye uhitaji maalum, huku kilele cha maadhimisho hayo kikitarajiwa kufanyika Juni 19, 2026 kwa kushirikisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali wa biashara.
Pamoja na hayo amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo, akisema yatatoa fursa ya kujifunza, kujenga ushirikiano wa kibiashara na kutangaza bidhaa pamoja na huduma zao.






Social Plugin