Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAHLISO YAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KULINDA HAKI YA WANAFUNZI KUFANYA MTIHANI



Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amemshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo aliyoyatoa kupitia Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, yanayozitaka taasisi za elimu nchini kutowazuia wanafunzi kufanya mitihani kwa sababu ya kushindwa kulipa ada kwa wakati.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kiliba amesema hatua hiyo ni ya kihistoria na yenye kuzingatia haki pamoja na ustawi wa wanafunzi, hasa wale wanaotoka katika mazingira yenye changamoto za kiuchumi.

Amesema mara nyingi wanafunzi wamekuwa wakijiandaa kwa muda mrefu kufanya mitihani yao, lakini hulazimika kukosa fursa hiyo kutokana na kushindwa kumaliza malipo ya ada, jambo ambalo limekuwa likiwaongezea msongo wa mawazo na kuathiri ndoto zao za kielimu.

Kwa mujibu wa Kiliba, maelekezo hayo ya Waziri Mkuu ni mwitikio wa moja kwa moja wa ombi lililowasilishwa na uongozi wa TAHLISO kwa Rais Samia Suluhu Hassan wiki chache zilizopita.

Katika mazungumzo hayo, viongozi wa wanafunzi walieleza changamoto wanazokumbana nazo baadhi ya wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu kunyimwa haki ya kufanya mitihani kutokana na madai ya ada.


Kiliba amesema TAHLISO inaamini kuwa elimu ni haki ya msingi na kwamba mwanafunzi hapaswi kuadhibiwa kwa changamoto za kifedha zinazotokana na hali halisi ya maisha ya familia yake.


Aidha, ametoa wito kwa taasisi zote za elimu ya juu nchini kutekeleza maelekezo hayo kwa vitendo na kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa mazingira bora ya kujifunza na kufanya mitihani yao bila vikwazo visivyo vya lazima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com