Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzania imefanikiwa kujenga Taifa lenye umoja, mshikamano na amani ndani ya kipindi cha zaidi ya miongo sita tangu kupata uhuru, akisisitiza kuwa nchi si mkusanyiko wa makabila bali ni Taifa moja lililounganishwa na misingi ya utaifa.
Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Mei 16, 2026 wakati akizungumza katika kongamano la wanafunzi wa vyuo lililofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, lenye kaulimbiu ya “Never Again: Tuipende, Tuitunze, Tuilinde Nchi Yetu”, lililoandaliwa na Jumuiya ya Serikali za Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).
Katika hotuba yake, Profesa Kabudi amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kutokana na uwezo wake wa kuunganisha wananchi wa makabila zaidi ya 120 pamoja na waumini wa dini tofauti chini ya misingi ya amani, mshikamano na uzalendo.
Aidha, amesisitiza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Tanzania ni Taifa la kidemokrasia lisilo na dini, jambo ambalo limeendelea kusaidia kudumisha usawa, uvumilivu na kuheshimiana miongoni mwa wananchi wake.
Amesema mafanikio hayo yametokana na misingi imara iliyowekwa tangu enzi za waasisi wa Taifa, waliotanguliza umoja wa kitaifa kuliko tofauti za kikabila, kidini au kikanda.
Profesa Kabudi ameongeza kuwa mshikamano wa Watanzania umeifanya nchi kuwa kinara wa amani na mtangamano wa kijamii katika bara la Afrika, huku akiwataka vijana kuendelea kuilinda, kuipenda na kuitunza nchi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Social Plugin