Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS DK. MWINYI AKEMEA MAKUNDI NDANI YA CCM


Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasihi viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuwa mstari wa mbele katika kuwaunganisha wanachama na kuimarisha mshikamano badala ya kuanzisha makundi yanayoweza kudhoofisha umoja wa chama.

Akizungumza katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu mkoani Kusini Unguja wakati wa ziara yake ya kuimarisha chama na kutoa shukrani kwa ushindi wa mwaka 2025, Dk. Mwinyi alionya kuwa baadhi ya viongozi wakiwemo wabunge, wawakilishi, na madiwani wamekuwa wakijihusisha na makundi yasiyofaa kwa ajili ya kulinda maslahi yao ya kisiasa.

Alisisitiza kuwa ingawa makundi ya kumuunga mkono mgombea ni jambo la kawaida wakati wa uchaguzi, mara baada ya mchakato kukamilika, makundi hayo yanapaswa kuvunjwa ili wanachama wote wabaki wamoja chini ya uongozi uliopo madarakani.

Dk. Mwinyi alifafanua kuwa si utamaduni wa CCM kwa viongozi kutoa zawadi au misaada kwa wanachama wachache wanaowaunga mkono huku wakiwatenga wengine, hali inayochochea malalamiko na migogoro isiyo ya lazima.

Alihimiza umuhimu wa chama kuimarisha uchumi wake kwa kuvutia wawekezaji katika rasilimali zake nyingi, ikiwemo sekta ya utalii na majengo ya biashara, ili kuendana na mifumo ya vyama rafiki vya ukombozi duniani kama ANC vyenye mafanikio makubwa kiuchumi.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi katika mwendelezo wa ziara ya Makamu Mwenyekiti ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa Dk.Mohamed Shein uliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

BAADHI ya Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakifuatilia hotuba ya Makamu Mwenyekiti katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wa Dk.Mohamed Shein uliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Aidha, aliitaka Kamati za Maadili za chama katika ngazi zote kutekeleza majukumu yao wakati wote kwa mujibu wa kanuni, badala ya kusubiri kuchukua hatua dhidi ya wanachama wakorofi wakati wa kipindi cha uchaguzi pekee.

Katika upande wa maendeleo ya kijamii, Rais Dk. Mwinyi alitangaza habari njema kwa wakazi wa Mkoa wa Kusini Unguja, akibainisha mpango wa serikali wa kujenga barabara ya kisasa ya njia nne kuanzia Tunguu hadi Makunduchi kwa ajili ya kuchochea biashara na ajira.

Aliongeza kuwa serikali imejipanga kumaliza changamoto ya maji safi na salama mkoani humo kupitia upanuzi wa mtandao wa usambazaji, huku akisisitiza kuwa katika awamu yake ya pili, ataendelea kuboresha maisha ya watu kama alivyoanza kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 300,000 hadi 500,000.

Alihitimisha kwa kusema kuwa ahadi zote za Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030 zitafanyiwa kazi kwa vitendo ili kukiwezesha chama kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 kikiwa na nguvu na ushindi wa kishindo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com