Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani na Jaji Mkuu Mstaafu, Profesa Ibrahim Hamis Juma, ametoa onyo dhidi ya utamaduni wa baadhi ya watu na vikundi kutaka kuminya maoni ya wengine, hususan katika mitandao ya kijamii.
Profesa Juma amesisitiza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka wazi kuwa kila mtu ana haki ya kuwa na maoni, hivyo ni jambo la hatari kwa kikundi fulani kutaka maoni yao pekee ndiyo yasikike huku wakiwashambulia wale wenye mtazamo tofauti.
Akizungumzia hali inayoendelea kwenye majukwaa ya kidijitali, baada ya ripoti ya tume ,Profesa Juma amebainisha kuwepo kwa watu wanaoshambuliwa kama "nyuki" pale tu wanapothubutu kutoa maoni yanayokinzana na matakwa ya kikundi fulani.
Amesema tabia hiyo haina afya kwa taifa linalokua kidemokrasia na ni jaribio la kuzuia matokeo ya utafiti na methodolojia ya kitaalamu ambayo tume imetumia kupata ukweli kutoka kwa Watanzania wa kada mbalimbali.
Profesa Juma amewakumbusha wadau wote wanaojipambanua kama waumini wa demokrasia na haki za binadamu kuwa, kipimo halisi cha imani hiyo ni utayari wa kusikiliza maoni ya wengine hata kama hayafurahishi.
Amesema ukitaka kupata unachotaka, lazima utambue na kuheshimu wanachotaka wengine ili kuepuka uharibifu, kwani huwezi kudai haki huku ukiwa unapora haki za wengine za kutoa maoni yao kwa uhuru.

Social Plugin