Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Halmashauri za Miji, Halmashauri za Wilaya, Shule za msingi, wadau wa mazingira pamoja na Mabalozi wa Mazingira, limepanda miche ya miti elfu arobaini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo.
Zoezi hilo limefanyika kupitia kanda 13 za NEMC nchi nzima huku likiambatana na utoaji wa elimu ya Uhifadhi na Usimamizi wa mazingira kwa wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa wa umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema Baraza hilo limekasimiwa wajibu na dhamana ya kuhifadhi na kusimamia mazingira kwa mujibu wa Sheria, hivyo lina wajibu wa kuhakikisha mazingira yanaendelea kulindwa kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo.
Dkt. Semesi amesema maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC yanalenga kuonesha mafanikio na dhamira ya Baraza hilo katika kusimamia mazingira kwa vitendo kupitia kampeni ya upandaji miti na utoaji wa elimu kwa jamii.
“Tunapoelekea maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa NEMC tunataka kuadhimisha kwa vitendo. Lengo letu ni kuiona Tanzania ya kijani na yenye hewa safi,” amesema Dkt. Semesi.
Aidha amesema kampeni hiyo pia inalenga kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusisitiza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili nchini.
Kanda za NEMC zilizoshiriki katika zoezi hilo ni pamoja na Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Kaskazini Arusha, Kanda ya Bagamoyo, Kanda ya Kusini Mtwara, Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Geita, Kanda ya Ziwa Victoria Mashariki Mwanza, Kanda ya Temeke, Kanda ya Ilala, Kanda ya Mashariki Kaskazini, Kanda ya Mashariki Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi Kigoma pamoja na Kanda ya Morogoro Rufiji, huku NEMC ikieleza kuwa zoezi hilo ni endelevu kwa maendeleo ya mazingira nchini















Social Plugin