
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewatembelea na kuwafariji wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zunzuli iliyopo Kata ya Mwenge, Wilaya ya Shinyanga, kufuatia tukio la kuungua kwa bweni la wanafunzi wa kike lililotokea Mei 6, 2026 wakati wanafunzi wakiwa wanaendelea na masomo.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Bi. Aisha Mwinshari, amesema kuwa licha ya moto huo kusababisha uharibifu mkubwa wa mali mbalimbali za wanafunzi na shule, hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika tukio hilo.
Ameeleza kuwa moto huo uliharibu vifaa muhimu vya wanafunzi ikiwemo magodoro, mashuka, sare za shule na mahitaji mengine ya msingi yaliyokuwa ndani ya bweni hilo.
Kwa upande wake, Mhe. Mhita amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imechukua hatua za haraka kutoa msaada wa vifaa vya awali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 15 ili kuwasaidia wanafunzi walioathirika kurejea katika mazingira bora ya masomo.
Msaada huo umejumuisha magodoro, mashuka na vyandarua pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 6 zilizokabidhiwa kwa uongozi wa shule kwa ajili ya ununuzi wa sare za shule na viatu kwa wanafunzi waliopoteza mali zao kutokana na ajali hiyo.
"Jambo muhimu zaidi ni kwamba watoto wetu wako salama. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanafunzi hawa wanapata mazingira mazuri ya kuendelea na masomo yao,” alisema Mhe. Mhita.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha bweni lililoungua linajengwa upya kwa kiwango cha kisasa ili kuboresha mazingira ya malazi kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Mgodi wa Busolwa Mining, Hamad Suleiman, amesema mgodi huo umeunga mkono jitihada za Serikali kwa kutoa zaidi ya magodoro 50 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi waliopata athari ya tukio hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Zunzuli, George Ulomi, alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa hatua za haraka alizochukua kufuatia tukio hilo, akisema msaada huo umeleta faraja kubwa kwa wanafunzi na kuongeza matumaini kwa jamii ya shule hiyo.
Amesema ushirikiano uliooneshwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ni ishara ya kujali ustawi na elimu ya watoto wa Mkoa wa Shinyanga.

















Social Plugin