Mbunge wa Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, Mhe. Azza Hilal Hamad akiwashukuru wananchi wa Kijiji cha Igalamya, Kata ya Usule kwa imani yao ya kumchagua yeye kuwa Mbunge, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais pamoja na madiwani wao katika uchaguzi mkuu. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, Mhe. Azza Hilal Hamad akisalimiana na mkazi wa kijiji cha Bunonga kata ya Mwamala wakati wa ziara yake jimboni
Mbunge wa Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza katika Zahanati ya kijiji cha Bunonga kata ya Mwamala ambayo upauaji wake umeanza
Burudani ya ngoma ya Ugoyangi ikiendelea wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, Mhe. Azza Hilal Hamad katika Kijiji cha Igalamya, Kata ya Usule.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, Mhe. Azza Hilal Hamad ameanza ziara maalum ya kuwashukuru wananchi kwa imani kubwa waliyoionesha kwa kumchagua kuwa Mbunge wa jimbo hilo pamoja na kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika ziara hiyo inayoambatana na mikutano ya hadhara katika kata mbalimbali za jimbo hilo, Mhe. Azza ameendelea kueleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia sekta za afya, miundombinu, maji na umeme.
Leo Mei 16, 2026, Mhe. Azza amekagua ujenzi wa upauaji wa Zahanati ya Kijiji cha Bunonga, Kata ya Mwamala, mradi uliojengwa kwa nguvu za wananchi huku hatua ya upauaji ikigharamiwa na fedha za Mfuko wa Jimbo kiasi cha shilingi milioni 15.
Mbali na hilo, mbunge huyo pia amekagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Usule – Buchama, mradi ambao umeanza kutekelezwa baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kutoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo muhimu ya miundombinu.

Akiwa katika ziara hiyo na kuongozana na viongozi wa CCM pamoja na viongozi wa Serikali, Mhe. Azza amesema Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa vitendo, huku akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi wa maeneo yote ya jimbo hilo.
“Changamoto za wananchi tunazifahamu na Serikali ipo kazini. Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma za umeme zinaendelea kusogezwa kwenye vitongoji mbalimbali. Tayari baadhi ya maeneo yamepata umeme na hatua za kusogeza huduma ya maji zinaendelea vizuri,” amesema Mhe. Azza.
Akizungumza katika eneo la ujenzi wa Zahanati ya Bunonga, Mhe. Azza ameitaka kamati inayosimamia mradi huo kuhakikisha inasimamia kikamilifu ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
“Tunataka wananchi waanze kupata huduma za afya mapema iwezekanavyo. Kamati isimamie mradi huu kwa umakini mkubwa. Hatutaki kuona mapungufu yoyote. Mkandarasi amelipwa fedha na vifaa vya ujenzi vimeletwa, hivyo hakuna mwananchi atakayetozwa fedha yoyote katika mradi huu,” amesema.
Aidha Mhe. Azza, ameiomba Serikali kuendelea kutoa ushirikiano ili kukamilisha mradi huo kwa wakati huku akiwataka wananchi kuendelea kuutunza mradi huo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kuhusu ujenzi wa Barabara ya Usule – Buchama, Mhe. Azza amesema kazi tayari imeanza ikiwemo utengenezaji wa madaraja ili kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora ya usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.
Katika mikutano yake ya hadhara, Mbunge huyo pia amekuwa akisikiliza na kupokea kero, maoni pamoja na ushauri kutoka kwa wananchi, huku akiahidi kuendelea kuwa kiungo madhubuti kati ya wananchi na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Itwangi.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
@malundeblog Mbunge wa Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad akikagua upauaji Zahanati ya Kijiji cha Bunonga kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kupauliwa kwa mfuko wa jimbo ..Ageuka mbogo mbao kutowekewa Dawa
♬ original sound - Malunde
@malundeblog SHUHUDIA ngoma ya Kisukuma ya Wagoyangi 'JAMAA ANACHEZA NA NYOKA" kutoka kijiji cha Sumbigu kata ya Bukene wakitoa burudani kwenye ziara ya Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe.Azza Hilal Hamad katika kijiji cha Igalamya kata ya Usule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga!
♬ original sound - Malunde














































































Social Plugin