Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI MABAO AWASHUKURU WANANCHI NGOGWA KWA KUMPA IMANI YA UONGOZI, CCM YASISITIZA AMANI NA USHIRIKIANO


Diwani wa Kata ya Ngogwa katika Manispaa ya Kahama, Abel Mabao, akiwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa imani waliomuonesha katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais uliofanyika Oktoba mwaka 2025

Na Neema Nkumbi, Kahama

Diwani wa Kata ya Ngogwa katika Manispaa ya Kahama, Abel Mabao, amewashukuru wananchi wa kata hiyo kwa imani waliomuonesha katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais uliofanyika Oktoba mwaka 2025, huku akiahidi kutowavunja moyo wananchi waliompa dhamana ya kuwa mwakilishi wao. 

Mabao amesema ataendelea kusimamia maslahi ya wananchi na kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Akizungumza mbele ya wananchi wa Ngogwa, Mabao amesema jukumu lake kubwa ni kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kata hiyo, akisisitiza kuwa ataendelea kupigania upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo maji, barabara na umeme ili kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema tayari ameanza kushirikiana na madiwani pamoja na viongozi wa serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa vitendo huku akibainisha kuwa baadhi ya maeneo tayari yameingizwa katika mipango ya bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kuanzia mwezi Julai mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Mabao ameipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka huduma za maendeleo kwa wananchi akitaja miradi ya maji, umeme pamoja na miundombinu kuwa ni miongoni mwa mafanikio yanayoonekana katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Ngogwa.

Diwani huyo pia amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na ushirikiano ili kuharakisha maendeleo ya kata hiyo, amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo na kwamba wananchi wanapaswa kushirikiana kwa karibu na viongozi wao ili kujenga jamii yenye ustawi na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila, amewataka wananchi kuendelea kulinda amani baada ya uchaguzi mkuu, akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii, amesema wananchi wa Kahama wameonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kushiriki uchaguzi kwa utulivu na kufanya maamuzi yao kwa amani.

Simbila amesema bila amani hakuna maendeleo, kwani hata biashara, uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo haviwezi kufanikiwa katika mazingira ya migogoro na vurugu.

Aidha, amegusia changamoto zinazoendelea kujitokeza duniani ikiwemo vita katika baadhi ya mataifa, akisema hali hiyo inaonesha umuhimu mkubwa wa kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini Tanzania.

Naye Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Elia Wikunge, amewapongeza wananchi wa Kata ya Ngogwa kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano na mshikamano katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo amesema ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wao ni msingi muhimu wa mafanikio ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa karibu na wananchi katika kusikiliza changamoto zao na kushirikiana nao kutafuta suluhisho la maendeleo endelevu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com