.mp4.00_00_21_14.Still007.jpg)
Katika kuimarisha harakati za kuhubiri amani na mshikamano wa kijamii, Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Mkoani Shinyanga imeanzisha kamati ndogo ndogo 17 zitakazosaidia kusimamia na kuratibu shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo ndani ya mkoa huo.
Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, amesema hatua ya kuunda kamati hizo inalenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi pamoja na kuhakikisha jumuiya hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia elimu ya amani, maridhiano na upendo.
Amesema kamati hizo zitakuwa na jukumu la kuratibu shughuli mbalimbali zinazohusu kuimarisha mshikamano wa kijamii, kuhamasisha maadili mema na kuendelea kujenga mazingira ya utulivu na ushirikiano miongoni mwa Watanzania.
Sheikh Balilusa ameongeza kuwa JMAT itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii inaendelea kuishi kwa amani na kuheshimiana bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa au kijamii.
Sheikh Balilusa amesema suala la maridhiano na amani ni jambo muhimu katika maisha ya kila mwananchi na kusisitiza kuwa jumuiya hiyo haibagui dini, kabila wala mila kwani imekusanya viongozi wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa kimila kwa lengo la kujenga umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Shinyanga, Stephano Tano amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kushikamana katika kulinda umoja wa taifa kama alivyoelekeza Hayati Julius Nyerere kuwa ulinzi wa taifa ni jukumu la kila mtanzania mzalendo.
Naye mjumbe wa kamati ya JMAT, Anna Mwalongo amesema amani ndiyo msingi wa maisha bora na maendeleo ya jamii, akieleza kuwa mali, familia na mafanikio yote hayana maana ikiwa hakuna amani nchini.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda tunu za taifa kwa kudumisha upendo, mshikamano na maridhiano ili kuendelea kuijenga Tanzania yenye umoja na utulivu.
.mp4.00_00_17_00.Still008.jpeg)
.mp4.00_00_28_17.Still006.jpeg)
Social Plugin