Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHEVRON YATANGAZA NIA YA KUWEKEZA SEKTA YA MAFUTA NA GESI TANZANIA


Kampuni kubwa ya nishati kutoka Marekani, Chevron Corporation imeeleza utayari wake wa kuwekeza nchini Tanzania katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, hatua inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji katika sekta ya nishati nchini.

Hayo yameelezwa leo, Mei 12, 2026 jijini London, Uingereza, wakati wa kikao kati ya viongozi wa kampuni hiyo na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), pembeni mwa mkutano wa Africa Energies Summit 2026 unaoendelea nchini humo.

Katika kikao hicho, Makamu wa Rais wa Chevron anayesimamia shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Bwana Kelvin McLachlan, alisema kampuni hiyo inaendelea kutafuta maeneo mapya ya kimkakati ya uwekezaji barani Afrika, huku Tanzania ikionekana kuwa miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa kutokana na utulivu wake wa kisiasa, mazingira rafiki ya biashara na uwepo wa rasilimali kubwa za gesi asilia.

Alieleza kuwa Chevron ina uzoefu mkubwa katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Nigeria, Angola na Equatorial Guinea na kwamba kampuni hiyo ina nia ya kupanua uwekezaji wake katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, aliieleza Chevron kuwa Tanzania imeendelea kuweka mazingira bora na thabiti ya uwekezaji katika sekta ya nishati hususani sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia kupitia mifumo imara ya kisheria, kisera na kiudhibiti inayolenga kulinda maslahi ya wawekezaji pamoja na nchi kwa ujumla.

Mhandisi Sangweni alibainisha kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia vilivyopo nchi kavu na baharini, huku Serikali ikiendelea kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo ili kuongeza ushindani na kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Aidha, alieleza kuwa maandalizi ya duru nyingine ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta yanaendelea, sambamba na jitihada za kuongeza upatikanaji wa data za petroli kupitia tafiti na uchukuaji wa taarifa za kijiolojia na kijiofizikia hatua zitakazosaidia kuongeza uwezekano wa ugunduzi wa mafuta na gesi asilia zaidi nchini.

Alisisitiza pia kuwa uwepo wa miundombinu ya usafirishaji na uchakataji wa gesi asilia, eneo iliyopo Tanzania kijiografia, utulivu wa kisiasa na mazingira bora ya uwekezaji yanaifanya Tanzania kuwa eneo la kimkakati kwa wawekezaji wakubwa kama Chevron.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa PURA aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kufungua fursa mpya za uwekezaji kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mradi wa gesi asilia iliyosindikwa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi (LNG) ambao unatarajiwa kuongeza thamani ya sekta ya nishati na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara ya gesi asilia katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Katika kikao hicho, pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa mazungumzo na ushirikiano wa karibu ili kuchochea uwekezaji, maendeleo ya teknolojia na ukuaji endelevu wa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com