Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZAZI WA CCM SHINYANGA MJINI WAADHIMISHA MIAKA 71 KWA KISHINDO, MAKOMBE AHIMIZA AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anorld Makombe akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo Wilaya ya Shinyanga Mjini katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Hamisa Chacha akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo Wilaya ya Shinyanga Mjini katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto.
Diwani wa Kata ya Kolandoto Mshagatila Moses akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Kibabi akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anorld Makombe, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kudumisha umoja na kuimarisha mshikamano wa kitaifa ili kuenzi misingi iliyoasisiwa na viongozi waasisi wa taifa.

Makombe ametoa wito huo leo Mei 9, 2026 wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo Wilaya ya Shinyanga Mjini katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto.

Amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na utulivu barani Afrika kutokana na misingi imara ya umoja na mshikamano iliyoasisiwa tangu enzi za waasisi wa taifa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha tunu hiyo inalindwa kwa nguvu zote.

“Tutunze amani yetu, tudumishe umoja na mshikamano wa kitaifa. Tanzania imeendelea kuwa kimbilio la mataifa mengine kutokana na hali ya amani iliyopo. Ni jukumu letu kuendelea kuilinda na kuiendeleza kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Makombe.
Ameongeza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yanapaswa kuwa funzo kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuendelea kuhubiri maridhiano, upendo na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi.

Katika hatua nyingine, Makombe amesisitiza umuhimu wa kulinda maadili na tamaduni za Kitanzania, akieleza kuwa familia na jamii zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya heshima, utu na uwajibikaji.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, akisema malezi bora ni msingi wa kujenga taifa lenye maadili na amani ya kudumu.
“Jumuiya ya Wazazi CCM ina jukumu kubwa la malezi katika jamii. Ni wajibu wetu sote kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yatakayowajenga kuwa wananchi wema wa baadaye,” amesema.

Makombe pia amewapongeza wananchi wa Shinyanga Mjini kwa kuendelea kuiamini CCM kupitia uchaguzi uliopita, huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi pamoja na madiwani wa CCM kwa ushindi walioupata.

Vilevile ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kutwaa tuzo ya kinara wa usafi wa mazingira kitaifa mwaka 2026, akisema mafanikio hayo yanaonyesha ushirikiano mzuri kati ya viongozi na wananchi katika kulinda mazingira na afya ya jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, amesema Jumuiya hiyo imeendelea kuwa imara tangu kuanzishwa kwake, huku akiwataka wanachama wa CCM kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na uadilifu.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Kibabi, amesema maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya hiyo yamekuwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa kijamii, malezi bora na huduma kwa makundi yenye uhitaji katika jamii.
Amesema katika kuadhimisha miaka hiyo, Jumuiya ya Wazazi imeendesha shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa elimu ya malezi bora kwa watoto, kufanya matendo ya huruma, kutembelea wagonjwa pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu kama sabuni na mafuta. 

“Tumegusa makundi mbalimbali katika jamii kwa kutoa misaada na kuhamasisha malezi bora kwa watoto ili kujenga kizazi chenye maadili mema na uwajibikaji,” amesema Doris.

Aidha, amesema Jumuiya hiyo imetoa chakula kwa watoto wa shule pamoja na kupanda miti 361 kama sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa Jumuiya ya Wazazi itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo ya jamii, ustawi wa wananchi na kuendeleza utamaduni wa kusaidiana na kushikamana katika jamii.
Aidha, katika maadhimisho hayo, Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini imetoa vyeti vya pongezi na zawadi kwa makundi mbalimbali kwa kutambua mchango wao katika kuimarisha shughuli za Jumuiya na maendeleo ya jamii.

Katika maadhimisho hayo Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Kolandoto imemkabidhi zawadi Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Kibabi, kwa kutambua utendaji wake mzuri wa kazi pamoja na ushirikiano wake ndani ya Jumuiya hiyo.

Naye Doris Kibabi amemkabidhi zawadi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, kama ishara ya kuthamini ushirikiano na mshikamano uliopo katika uongozi wa Jumuiya hiyo.

Aidha, katika kuadhimisha miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi CCM, viongozi na wanachama wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Shinyanga Mjini wameshiriki zoezi la upandaji miti katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Kibabi akikabidhiwa zawadi kwenye maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo Wilaya ya Shinyanga Mjini katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com