Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anorld Makombe, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kudumisha umoja na kuimarisha mshikamano wa kitaifa ili kuenzi misingi iliyoasisiwa na viongozi waasisi wa taifa.
Makombe ametoa wito huo leo Mei 9, 2026 wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo Wilaya ya Shinyanga Mjini katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto.
Amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na utulivu barani Afrika kutokana na misingi imara ya umoja na mshikamano iliyoasisiwa tangu enzi za waasisi wa taifa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha tunu hiyo inalindwa kwa nguvu zote.
“Tutunze amani yetu, tudumishe umoja na mshikamano wa kitaifa. Tanzania imeendelea kuwa kimbilio la mataifa mengine kutokana na hali ya amani iliyopo. Ni jukumu letu kuendelea kuilinda na kuiendeleza kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Makombe.
Ameongeza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yanapaswa kuwa funzo kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuendelea kuhubiri maridhiano, upendo na mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi.
Katika hatua nyingine, Makombe amesisitiza umuhimu wa kulinda maadili na tamaduni za Kitanzania, akieleza kuwa familia na jamii zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya heshima, utu na uwajibikaji.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, akisema malezi bora ni msingi wa kujenga taifa lenye maadili na amani ya kudumu.

Social Plugin