Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo(Mb), amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Jamhuri ya Seychelles Mhe. Barry Faure pembezoni mwa Mkutano wa Tisa Bahari ya Hindi jijini Port Louis, Mauritius Aprili 11,2026.
Kikao hicho, kililenga kuangalia njia za kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Seychelles ambapo viongozi hao pia walijadili masuala mbalimbali ya maslahi ya pamoja ikiwemo ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, na amani ya kikanda.
Tanzania na Seychelles zinashirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji. Bidhaa kuu zinazouzwa Nje ni pamoja na misumari, pini ndogo (tacks), pini za kuchomelea misumari ya bati vikolezo na bidhaa zinazofanana, bidhaa za chuma au chuma kigumu, nati nazi na korosho ambapo bidhaa kuu zinazoagizwa ni nguo, samaki wa jamii ya jodari, na jodari aina ya skipjack.
Kuhusu uwekezaji katika kipindi cha kuanzia 2014 hadi 2024 Tanzania na Seychelles zimekuwa zikishirikiana katika ujenzi wa majengo ya biashara na viwanda na hivyo kusababisha ajira nchini. Tanzania na Seychelles pia zimekuwa zikishirikiana katika eneo la ulinzi na usalama pamoja na masuala ya magereza.
Mawaziri hao walielezea dhamira ya kutumia matokeo ya kikao chao kuendelea kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya biashara, utalii na usalama, kwa lengo la kukuza maendeleo na kudumisha amani, utulivu na usalama katika ukanda wa Bahari ya Hindi.






Social Plugin