Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Mohamed Abu Bakar Saleh Fattah jijini Port Louis, Mauritius ili kuongeza ushirikiano katika Biashara, Nishati na Masuala ya Kikanda na kimataifa kwa manufaa ya pande mbili.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili namna ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Misri, uliojengwa na misingi ya kihistoria ya urafiki na ushirikiano wa muda mrefu na waasisi wa nchi zao.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wamesisitizia umuhimu wa kuongeza ushirikiano katika sekta za kiuchumi, hususan biashara, uwekezaji, nishati, miundombinu na maendeleo ya viwanda, ili kukuza uchumi wa nchi zao kwa manufaa ya wananchi wake.
Aidha, walibadilishana mawazo na uzoefu kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa yanayoathiri Bara la Afrika, na kukubaliana juu ya haja ya kuimarisha mshikamano wa nchi za Afrika katika kukabiliana na changamoto za pamoja kama vile mabadiliko ya tabianchi, usalama wa kikanda na maendeleo endelevu.
Viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano ndani ya majukwaa ya kimataifa na kikanda, kuunga mkono juhudi za maendeleo ya uchumi wa buluu na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Waziri Kombo na Naibu Waziri Fattah wapo nchini Mauritius kushiriki Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi unaofanyika kuanzia Aprili 10 hadi 12, 2026 ambapo viongozi kutoka nchi zinazopakana na bahari ya Hindi wanajadiliana na wadau mbalimbali kuhusu fursa za kiuchumi, usalama wa bahari na ushirikiano wa kikanda katika eneo hilo.












Social Plugin