
Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wamepokea kwa mtazamo chanya ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani, wakieleza kuwa inaweza kuwa chachu ya kuimarisha umoja, amani na maridhiano nchini. Wananchi hao wamesema wanaamini kuwa utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo utasaidia kurejesha mshikamano wa kitaifa na kuzuia kujirudia kwa matukio ya uvunjifu wa amani siku zijazo.
Akizungumza kuhusu ripoti hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume, Mohamed Chande Othman, mmoja wa wakazi wa Shinyanga Mjini, Chief Abdallah Sube, amesema ameipokea vizuri kwa kuwa inalenga kuponya majeraha yaliyosababishwa na matukio ya uvunjifu wa amani.
“Nimeipokea vizuri ripoti, inasaidia kuponya. Sisi Watanzania tumepata uhuru kwa njia ya mazungumzo, siyo kwa vita. Hivyo ripoti hii inatusaidia kukaa pamoja na kufanya maridhiano ili tuendelee kuwa salama,” amesema Sube.
Ameongeza kuwa ni wakati wa wananchi kurejea kwenye misingi ya mazungumzo kwa lengo la kuondoa tofauti zilizojitokeza na kusababisha migogoro, akisisitiza umuhimu wa kusahihishana pale walipokosea.
“Turudi mezani kwa ajili ya mazungumzo ya wazi na ya kujenga ili kuondoa tofauti zilizojitokeza na kusababisha uvunjifu wa amani. Kupitia mchakato huo, tuimarishe umoja wetu na kuwa kitu kimoja tena kama Watanzania. Wale tuliokoseana, ni vyema tukutane, tuzungumze kwa utulivu na kusahihishana pale tulipokosea kwa lengo la kujenga mustakabali bora wa taifa letu.” ameongeza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sababu kuu zilizochangia ghasia hizo ni pamoja na mchanganyiko wa malalamiko ya kisiasa, changamoto za kiuchumi pamoja na utendaji usioridhisha wa baadhi ya watumishi wa umma.
Ripoti hiyo imekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 23 Aprili 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kutafuta suluhu ya kudumu na kuimarisha amani nchini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com
Social Plugin