Mchambuzi wa masuala ya siasa Bw. Said Miraji amesema ripoti ya Tume huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imehimiza kuhusu uwajibikaji, ikitafsiri pia shida na matakwa ya wananchi na kutaka uwajibikaji wa pamoja katika kushughulikia changamoto zilizopo kwenye nyanja zote.
"Ile ripoti imegusa maeneo yote kuanzia watumishi wa umma katika uwajibikaji, imegusa Vyombo vya usalama katika matumizi ya nguvu na mambo mengine na zaidi ripoti hii imegusa mpaka wanasiasa kwa kaulimbiu zao akiwaambia nao wamekuwa sababu ya tatizo hilo wakisahau kuwa kuna watu wanawaamini na kuwafuata." Amesema Bw. Miraji.
Mchambuzi huyo amebainisha hayo siku mbili mara baada ya Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande kutoa ripoti yake kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo pamoja na mambo mengine ilieleza kuhusu mapendekezo yake na namna ambavyo baadhi ya mambo yalivyochangia kutokea kwa ghasia na mauaji ya raia mnamo Oktoba 29, 2025.
Bw. Miraji ameeleza pia namna ripoti hiyo ilivyozungumzia changamoto zilizojikusanya kwa muda mrefu ikiwemo changamoto za ajira na hali ngumu ya maisha, akisema ikiwa ripoti na mapendekezo ya Tume hiyo yatafanyiwa kazi huenda ikawa ni suluhu ya mgawanyiko na changamoto ambazo jamii inapitia kwa hivi sasa.

Social Plugin