Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UFUNGUZI WA LIGI YA UVCCM BUKOBA CUP WAFANA, VIJANA WATAKIWA KUDUMISHA AMANI NA UMOJA

Na Mbuke Shilagi Kagera. 

Ligi ya UVCCM Bukoba Cup imefunguliwa rasmi Aprili 24, 2026 katika Uwanja wa Kaitaba, huku ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali na mamia ya vijana wa Manispaa ya Bukoba. 

Ufunguzi huo umefanywa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Faris Buruhan, ambaye amesisitiza umuhimu wa michezo kama nyenzo ya kuunganisha vijana na kujenga mshikamano wa kijamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Buruhan amempongeza Mwenyekiti wa UVCCM  Manispaa ya Bukoba Bw. James Michael Nyamanza kwa ubunifu wa kuwaleta pamoja vijana wa Kata zote za Manispaa ya Bukoba kupitia michezo, akieleza kuwa huu ni muda muafaka wa kuelekeza nguvu katika maendeleo baada ya kipindi cha uchaguzi. 

“Sasa ni wakati wa kufanya kazi kwa vitendo na Michezo hii iwe chachu ya kuimarisha umoja, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa vijana wetu,” amesema.

Aidha, amewataka waamuzi na waandaaji wa mashindano hayo kusimamia haki na weledi ili kuhakikisha ushindani unakuwa wa haki kwa kila timu.

Pia ametoa wito kwa vijana kuendelea kudumisha amani ya nchi, akisisitiza kuwa michezo hiyo inapaswa kuunganisha vijana wote bila kujali itikadi za vyama au tofauti za dini.

“Watanzania tunaunganishwa na utaifa wetu, siyo vyama wala dini, Ni muhimu mashindano haya yakazingatia usawa, na yasiwe na aina yoyote ya ubaguzi katika ngazi ya kata,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Buruhan amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo.

 Katika kuonyesha dhamira hiyo, amechangia kiasi cha shilingi milioni moja kusaidia mashindano hayo, huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kadri mashindano yatakavyoendelea.

Ufunguzi huo umepambwa na burudani mbalimbali, kabla ya mchezo wa kwanza uliowakutanisha wenyeji Bilele dhidi ya wageni Kashai, Katika mchezo huo wa kusisimua uliochezwa kwa dakika 90, timu ya Kashai iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bilele, na hivyo kuwanyamazisha wenyeji katika Uwanja wa Kaitaba.

Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano hayo, jumla ya timu 14 kutoka Kata za Manispaa ya Bukoba zinashiriki hatua ya makundi, ambapo kila timu itacheza mechi za nyumbani na ugenini, Timu saba zitakazomaliza juu ya makundi yao zitafuzu moja kwa moja kwenda hatua ya robo fainali.

Nafasi ya nane ya kukamilisha timu zitakazoingia robo fainali itachukuliwa na timu bora zaidi iliyoshika nafasi ya pili (best loser), itakayopatikana kwa kuzingatia alama nyingi zaidi, tofauti ya mabao na mabao ya kufunga.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com