Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI NI RASILIMALI MUHIMU KWA MAENDELEO YA NCHI, TUILINDE- MANGU



Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Ernest Mangu, ametoa wito kwa Watanzania kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake kuendeleza mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa amani ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyochapishwa na gazeti la Uhuru, Mangu alisema kuwa ishara zozote za kuchochea vurugu au kuvuruga utulivu wa nchi zinapaswa kukemewa mapema, akionya kuwa gharama za kupoteza amani ni kubwa na huathiri sekta zote za uchumi na ustawi wa jamii.

“Tuna wajibu wa kulinda amani yetu. Historia inaonyesha kuwa pale amani inapovunjika, athari zake huwa pana, zikigusa uchumi, uwekezaji na maisha ya watu kwa ujumla,” alisema.

Mangu alieleza kuwa Tanzania imejijengea sifa ya kuwa nchi yenye utulivu kwa muda mrefu, hali ambayo imeiwezesha kuvutia uwekezaji na kukuza shughuli za kijamii na kiuchumi. Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuendelezwa kupitia uwajibikaji wa wananchi na taasisi zote.

Kwa mujibu wake, baadhi ya mienendo inayoibuka katika jamii, ikiwemo matumizi mabaya ya majukwaa ya mawasiliano na kauli za uchochezi, inaweza kuhatarisha mshikamano uliopo kama haitadhibitiwa kwa wakati.

“Amani si jambo la kubahatisha. Inahitaji nidhamu, utii wa sheria na ushirikiano wa wananchi wote. Pale ambapo kuna dalili za kuvurugika kwa utulivu, hatua zichukuliwe haraka kuzuia madhara makubwa,” aliongeza.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa vyombo vya dola kufanya kazi kwa weledi na haki, akibainisha kuwa utekelezaji sahihi wa sheria ni nguzo muhimu ya kulinda utulivu wa nchi. Alisema wananchi wanapaswa kuwa na imani na taasisi za usalama na kushirikiana nazo katika kudumisha amani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com