Na John Mapepele, New York- Marekani.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa matumizi sahihi ya teknolojia na utafiti yana nafasi kubwa katika kushughulikia changamoto za idadi ya watu na kuharakisha maendeleo endelevu.

Akizungumza katika Mkutano wa 59 wa Idadi ya Watu na Maendeleo kinachofanyika New York nchini Marekani Aprili 13-17/ 2026, Mchengerwa amesema Tanzania inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yanawanufaisha wananchi wote.

“Ni heshima kubwa kuhutubia mkutano huu kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mchengerwa, akisisitiza kuwa serikali inapongeza mjadala wa kimataifa unaolenga kuunganisha teknolojia, utafiti na maendeleo ya watu.

Ameeleza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa kutumia vyema idadi kubwa ya vijana kama fursa ya kukuza uchumi.

“Kutumia kikamilifu nguvu ya vijana wetu ni msingi muhimu wa kufikia ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu,” alisisitiza.


Mheshimiwa Mchengerwa ameeleza kuwa, masuala ya idadi ya watu yamejumuishwa katika mipango ya maendeleo ya taifa ikiwemo Dira ya Maendeleo ya 2050 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, hatua inayolenga kuendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alibainisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya teknolojia, akitaja upanuzi wa miundombinu ya kidijitali kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mradi wa Tanzania ya Kidijitali. Alisema uwekezaji huo umeongeza upatikanaji wa huduma za serikali mtandao na kukuza ujuzi wa kidijitali hasa vijijini.

“Hatua hizi zinawezesha ushiriki mpana katika uchumi wa kidijitali huku tukihakikisha usalama wa taarifa na mifumo ya mawasiliano,” aliongeza.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa takwimu sahihi katika kupanga maendeleo, akitaja mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 pamoja na maboresho ya mfumo wa usajili wa vizazi na vifo (CRVS).
Katika sekta ya afya, Mchengerwa alisema serikali inaendelea kutekeleza huduma ya afya kwa wote kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia kama tiba kwa njia ya mtandao na mifumo ya kidijitali yameboresha utoaji wa huduma.

“Tunaendelea pia kuboresha afya ya mama na mtoto kupitia uwekezaji katika huduma za uzazi salama na huduma za dharura,” alisema.


Kuhusu usawa wa kijinsia, Mchengerwa alisema serikali inaendelea kupambana na ukatili wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi pamoja na sekta za sayansi na teknolojia.

Akizungumzia vijana, alieleza kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania ni vijana, hivyo Serikali inawekeza katika elimu, ujuzi na ajira ili kunufaika na nguvu kazi hiyo.

“Tunaimarisha elimu ya sayansi na teknolojia pamoja na programu za ubunifu na ujasiriamali kwa vijana,” alisema.


Kwa upande wa ushirikiano wa kimataifa, Mchengerwa alitoa wito kwa nchi mbalimbali kuimarisha ushirikiano na kubadilishana teknolojia ili kusaidia nchi zinazoendelea.

“Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanaleta matokeo chanya kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisisitiza.

Alihitinisha kwa kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kuhakikisha maendeleo jumuishi: “Tutaendelea kujitolea kuhakikisha hakuna mtu anayebaki nyuma.”