Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKAZI MWABOMBA WATAKA AMANI IDUMU: DARAJA LATHIBITISHA MATOKEO YA UTULIVU


Mkazi wa Mwabomba, Juma Mwendesha Nigula

**
Wakazi wa Kijiji cha Mwabomba, Kata ya Idahina Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, wamewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi ili kuwezesha utekelezaji endelevu wa miradi ya maendeleo, wakieleza kuwa mafanikio yanayoonekana yametokana na mazingira ya utulivu yaliyopo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mkazi wa Mwabomba, Juma Mwendesha Nigula, amesema uwepo wa Daraja la Mwabomba linalounganisha Masumbwe (Geita) na Mwabomba (Shinyanga) ni ushahidi wa wazi kuwa bila amani, miradi mikubwa ya maendeleo isingeweza kutekelezwa. 

Amesema hapo awali walipata mateso makubwa wakati wa masika kutokana na daraja la zamani kufunikwa na maji, lakini sasa hali imebadilika na kuleta unafuu mkubwa kwa wananchi.

“Kipindi cha masika daraja la mwanzo lilikuwa linafunikwa na maji mengi, hali iliyokuwa ikitutesa sana. Leo tunatoa shukrani kwa mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi. Sasa tunavuka bila hofu,” amesema Nigula.

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, wamehimiza wananchi kuendelea kudumisha mshikamano, amani na utulivu ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.

 Wamesema Daraja la Mwabomba ni mfano hai wa mafanikio yanayotokana na sera thabiti na hali ya amani, wakisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kulinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com