Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZABUNI RUVUMA, IRINGA NA NJOMBE WAJENGEWA UWEZO MATUMIZI YA MODULI YA RUFAA



Na Mwandishi Wetu, Songea na Iringa

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewakutanisha wazabuni na Taasisi Nunuzi wa mikoa ya Ruvuma, Iringa na Njombe na kuwajengea uwezo kuhusu Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na rufaa kwenye mfumo wa NeST kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa nyakati tofauti katika miji ya Songea na Iringa yamewahusisha washiriki 380 ambao ni wazabuni, wataalamu wa ununuzi, sheria, Tehama pamoja na makundi maalum yakiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye mahitaji maalum pamoja na mafundi wa ndani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amesema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa na PPAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kuwajengea uwezo wazabuni na Taasisi Nunuzi ili kuwapa ufanisi zaidi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, hususan katika kushughulikia malalamiko na migogoro itokanayo katika michakato ya ununuzi wa Umma.

“Mafunzo haya yanalenga kuimarisha utendaji kazi wenu, kuhakikisha ufanisi, kuongeza uelewa wa matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST),” amesema Bw. Sando

Bw. Sando ameongeza kuwa, katika kutimiza azma ya Serikali mafunzo yamewashirikisha vijana, wanawake na makundi maalum katika ununuzi wa umma ili kuwawezesha kupata elimu kuhusu ununuzi wa Umma hususan katika michakato ya ununuzi na kuhakikisha kuwa wanaisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi ya kimkakati yenye tija kwa Taifa.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amewasihi washiriki kutumia mafunzo hayo kujifunza namna moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa inavyofanya kazi katika Mfumo wa NeST kwani inatoa njia rahisi, ya haraka na yenye uwazi kwa wadau wote kushiriki katika mchakato wa ushughulikiaji wa malalamiko yanayotokana na michakato ya zabuni za umma.

“Matumizi ya moduli yameongeza ufanisi katika usimamizi wa rufaa, kupunguza muda wa kushughulikia mashauri, na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki, kuokoa muda na kupunguza gharama zinazohusiana na usuluhishi wa migogoro ya ununuzi,” ameongeza Bw. Sando

Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Sheria (PPAA), Bi. Florida Mapunda amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa Umma kuhusu taratibu za uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.

“PPAA kwa kushirikiana na PPRA tumejenga moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ili kuwasaidia wadau wa ununuzi wa umma (Wazabuni na Taasisi za Umma) kuwasilisha malalamiko na rufaa kwa ufanisi zaidi kupitia mtandao,” amesema Bi. Mapunda.

Bi. Mapunda ameongeza kuwa tangu kuanza kwa matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST, takribani mashauri 596 yamewasilisha kupitia mfumo huo, jambo linaloifanya Mamlaka ya Rufani kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa umma ili waweze kufahamu namna sahihi ya matumizi ya moduli hiyo.

Kupitia mafunzo hayo, mada zilizowasilishwa ni pamoja na uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa katika ununuzi wa umma, uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko katika mfumo wa NeST, utoaji wa tuzo, uandaaji, upekuzi, na utiaji saini wa mkataba.

Mada nyingine zilizowasilishwa ni uwasilishaji na ushughulikiaji wa maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha rufaa nje ya muda pamoja na uwasilishaji na ushughulikiaji wa rufaa katika mfumo wa NeST.

Mafunzo kuhusu Matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na Rufaa katika Mfumo wa NeST yaligawanyika katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Songea, Mkoani Ruvuma (tarehe 02 na 03 Machi, 2026) na awamu ya pili ilifanyika Iringa mjini, kwa mikoa ya Iringa na Njombe (tarehe 05 na 06 Machi, 2026).

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya awali yaliyofanyika katika Kanda ya Pwani, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Kanda ya Kati, mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kilwa, Lindi na Mtwara.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com