Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI NGORONGORO WAIOMBA SERIKALI KUTOA RIPOTI ZA TUME YA RAIS KUHUSU MIGOGORO YA ARDHI


Wananchi wa jamii ya Wamaasai wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha wameiomba Serikali kuharakisha kutolewa kwa ripoti za tume mbili zilizoundwa kuchunguza migogoro ya ardhi katika eneo hilo, wakieleza kuwa kuchelewa kwa taarifa hizo kumeongeza wasiwasi miongoni mwa wakazi.

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Machi 5, 2026, wananchi hao wamesema bado wanasubiri kwa hamu majibu kutoka kwenye tume hizo ambazo ziliundwa Februari 2025 kwa lengo la kuchunguza kwa kina migogoro ya ardhi inayojitokeza katika eneo la Ngorongoro.

Pamoja na hilo, tume hizo pia zilipewa jukumu la kutathmini mpango wa kuhamisha baadhi ya wakazi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomera kilichopo mkoani Tanga, hatua ambayo imekuwa ikizua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi.

 Pia Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tume hizo zilipewa muda wa siku tisini kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti kwa Serikali, ambapo muda huo ulitarajiwa kumalizika Mei 2025. Hata hivyo, hadi sasa ripoti hizo bado hazijawekwa wazi jambo ambalo limezua sintofahamu kwa wakazi wa eneo hilo.

 Aidha Wananchi wamesema kuchelewa kwa ripoti hizo kunazidi kuongeza hofu na mashaka, huku wengi wakitarajia majibu yatakayosaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiathiri maisha yao kwa muda mrefu.

Wameitaka Serikali kuhakikisha kuwa maamuzi yatakayofanyika yanazingatia maoni ya wananchi wa Ngorongoro, pamoja na kulinda haki zao za msingi na ustawi wa maisha yao.

Hata hivyo, wananchi hao wameeleza kuwa wanatarajia majibu ya wazi na yenye kuleta matumaini, ili hatimaye kupatikana kwa njia sahihi ya kumaliza changamoto za ardhi zinazolikabili eneo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com