Na mwandishi wetu, Dar
Watanzania wamehimizwa kuwa wazalendo, kuilinda na kuitetea nchi yao dhidi ya wale wanaotanguliza maslahi binafsi mbele na kueneza chuki kwa Watanzania, tahadhari ikitolewa pia kuhusu matumizi sahihi ya Mitandao ya kijamii kwa kuzingatia historia ya namna ambavyo Mitandao hiyo imetumika kama sehemu ya kueneza chuki na hasira ili kugombanisha wananchi katika Mataifa mbalimbali kote duniani.
Kauli hiyo imetolewa na mchambuzi wa masuala ya kiusalama Bw. Richard Mabele wakati wa mjadala wa Vijana na amani, akisisitiza rejea za Mataifa mbalimbali ambayo mpaka hii leo yamekuwa yakihangaika kurejesha amani yake ikiwemo Taifa la Libya ambalo raia wake wameteseka, kuhangaika na kutopea kwenye umaskini mkubwa mara baada ya kushawishiwa kuiondoa madarakani serikali ya mwanamapinduzi na Rais wake Bw. Muammar Muhammad Abu Minyar al-Gaddafi.
"Kuna mataifa mengi sana ambayo amani imekuwa sababu ya kuangushwa kwa tawala zake. Mitandao ilitumika kusambaza taarifa za uongo na za chuki mpaka watu wakajawa na hasira, wakaingia mtaani na wakaleta fujo. Wakati nasoma masuala ya usalama na uchunguzi nilikuwa na wanafunzi wanatoka Libya, wengi walikuwa wanajuta walichokuwa wanakifanya wenyewe kwenye nchi zao. Nchi yao sasa imevurugika na Walibya wenyewe wameangamiza jitihada zao za maendeleo." Amesema Bw. Mabele.
Mabele amesisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki na kuwa mstari wa mbele katika ulinzi wa amani ya Tanzania, akihimiza kila Mtanzania kumkataa na kuwakataa wale ambao wamekuwa na viashiria vya kuvunja amani ya Tanzania, akitahadharisha pia wapo wenye maslahi binafsi ambao wamekuwa wakilenga rasilimali za nchi, wakiamini kuwa hakuna namna ambavyo wanaweza kuzifaidi bila ya kuwavuruga watanzania na kusambaratisha amani ya Tanzania.

Social Plugin