Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC CHALAMILA AWAPA WIKI MOJA WAPORAJI ARDHI NA MATAPELI DAR ES SALAAM


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa muda wa wiki moja kuanzia Machi 2, 2026 kwa makundi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya utapeli na unyang’anyi wa mali, ikiwemo ardhi, kujisalimisha na kurejesha mali walizochukua kwa wamiliki halali.

Amesema Serikali ya Mkoa huo imejipanga kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaokiuka agizo hilo baada ya muda uliotolewa kumalizika.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia ziara yake katika Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambapo imebainika kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya utapeli na uporaji wa mali. Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mbinu ya kukodisha maeneo kisha kuyamiliki kwa njia ya udanganyifu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Chalamila amesema Serikali imebaini kiwango kikubwa cha utapeli wa ardhi unaosababisha mateso kwa wananchi, hususan makundi maalum kama wajane na warithi wa mali.

Ameongeza kuwa, Serikali pia imegundua uwepo wa matukio ya utapeli katika showroom za magari, ambapo baadhi ya wananchi hulipia magari lakini hawapati huduma, wakipewa visingizio kuwa magari yao bado yapo bandarini.

Vilevile, ameeleza kuwepo kwa mikopo isiyo na tija inayowaumiza wananchi kutokana na masharti magumu, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo.

Aidha, Mhe. Chalamila ametoa wito kwa wananchi wote waliotapeliwa au kudhulumiwa mali zao kuwasilisha malalamiko yao ofisini kwake ndani ya muda wa wiki moja, ili yaweze kufuatiliwa kabla ya kuanza kwa ziara maalum ya kushughulikia migogoro hiyo itakayoanza Machi 9, 2026.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Mahakama pamoja na TAKUKURU kwa juhudi zao katika kushughulikia kesi za aina hiyo. Hata hivyo, ametoa tahadhari kwa baadhi ya wasimamizi wa mirathi wanaouza mali za warithi halali kwa kisingizio cha kuwalea au kuwasomesha watoto wa marehemu, hali inayosababisha baadhi ya warithi kunyimwa haki zao.

Wakati huo huo, Mhe. Chalamila amezungumzia ujio wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayetarajiwa kuwasili mkoani Dar es Salaam Machi 3, 2026, ambapo atazindua matanki ya kuhifadhi mafuta katika Wilaya ya Kigamboni.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumuunga mkono Rais huyo wakati wa ziara yake muhimu kwa maendeleo ya taifa.











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com