Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. SHEMDOE AWAASA WALIMU 150 KUZINGATIA MAFUNZO NCHINI INDIA ILI KUWA MAHIRI NA KULETA MAGEUZI YA ELIMU NCHINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka walimu 150 wa Amali za Kihandisi wanaokwenda India kuongeza umahiri kuhakikisha wanajifunza kwa bidii ili watakaporejea wawajengee uwezo walimu wengine, na hatimaye kutoa mchango utaokuwa na tija katika kuharakisha mageuzi ya elimu nchini.

Prof. Shemdoe ametoa wito huo Machi 26, 2026 kwa walimu hao waliopata fursa ya kwenda nchini India kuongeza umahiri, wakati wa hafla ya kuwaaga walimu hao iliyofanyika Jiji Dar es Salaam.

“Nendeni mkajifunze kwa bidii na nidhamu, mkazingatie maadili, jifunzeni mbinu mpya na muwe tayari kuzitumia mtakaporejea, hivyo tunatarajia mtakaporejea mtakuwa nguzo ya kuboresha elimu ya amali katika shule zenu na chanzo cha maarifa kwa walimu wengine,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesisitiza kuwa mpango wa mafunzo hayo ni utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima ya miaka 10, unaolenga kujenga umahiri wa ufundishaji na kuandaa kizazi cha wataalamu wenye ushindani wa kimataifa, huku akiwataka walimu hao kutambua nafasi yao kama daraja kati ya sera na utekelezaji darasani.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia walimu hao fursa ya mafunzo, akisisitiza kuwa ni ishara ya dhamira ya dhati ya kuendeleza mageuzi ya elimu, huku akipongeza mshirikiano wa viongozi wa wizara za kisekta katika kulitekeleza kwa ufanisi.

Wanufaika wa mafunzo hayo, akiwemo Mwalimu Judith Faustine wa Uhandisi Ujenzi katika Shule ya Sekondari Mwadui Ufundi na Mwalimu Jacob Mwalyego wa fani ya Uashi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mbogwe, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia nafasi hii ya kipekee. Wamesema ni heshima kubwa na fursa ya kuongeza maarifa yatakayowawezesha kuendeleza mageuzi ya elimu nchini.

Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa ameeleza kuwa mafunzo hayo ya mwezi mmoja yamewahusisha walimu kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na viongozi wa ngazi ya elimu mkoa kutoka mikoa tisa, hivyo
kuiwezesha Tanzania kuandika ukurasa mpya katika historia ya elimu ya ufundi kwa kupeleka walimu 150 wa Amali za Kihandisi nchini India ambao  wakirejea watasimamia kikamilifu uendelevu wa mafunzo nchini.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com